Watoto sita wameuawa na wanne wamejeruhiwa kwa kucharangwa kwa panga na mwanamke aliyejulikana kwa jina la Nana Maganga (35 ) anayedaiwa kuwa na matatizo ya akili.
Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa kijiji cha Luzuko kata ya Mizibaziba wilaya ya Nzega Mkoani Tabora, naye aliuawa wakati akidhibitiwa na wananchi.
Imeelezwa kuwa tukio hilo limetokea majira ya saa 11 alfajiri juzi. Aidha imefafanuliwa kuwa kati ya watoto hao sita, watano ni wa kwake mwenyewe na mmoja ni mtoto wa kaka yake.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora Emmanuel Nley akithibitisha kutokea kwa mauaji ya watu hao, alisema Nana kutokana na tatizo lake la ugonjwa wa akili alikwenda kwa mganga wa jadi ambaye ni shemeji yake kwa lengo la kupatiwa matibabu ndipo mkasa huo wa kuwakata kwa panga watoto wake ambao alikuwa amelala nao katika chumba kimoja ulipotokea.
Kamanda Nley alisema kuwa waliomdhibiti Nana wakati akitekeleza mauaji hayo akiwemo shemeji yake, walidai walimdhibiti kwa kumfunga kamba ambapo baadaye mwenyewe alikunywa sumu na kupoteza maisha, jambo ambalo hata hivyo, kamanda Nley amelikanusha.
Alisema jeshi la polisi linawashikilia watu watano akiwepo mume wa Nana na mganga wa jadi kwa tuhuma za kumuua Nana na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kujua nini chanzo cha mauaji hayo ambayo yamesababisha vifo vya watoto wadogo wasiokuwa na hatia.
Aliwataja watoto hao kuwa ni pamoja na Pala Massanja(3), Shija Dotto (2), Nyawele Dotto(2) Sida Dotto(5), Kulwa Dotto (4) Dotto Dotto (4) pamoja na Nana.
Aidha, aliwataja watoto wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Kundi Dotto, Nembwa Dotto, Milembe Massanja pamoja na Mwashi Massanja.
Social Plugin