Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAREKANI YATISHIA KUIWEKEA UTURUKI VIKWAZO VIPYA IKINUNUA MFUMO WA MAKOMBORA WA S-400 KUTOKA URUSI

Uhusiano wa Marekani na Uturuki umekumbwa na msuguano mkubwa hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli ya Julai 2016. 



Baada ya Uturuki kusambaratisha mapinduzi hayo, ilisema kuwa Marekani ilihusika katika njama hiyo na kwa msingi huo uhusiano wa nchi hizo mbili uliingia baridi.

Kinyume na matumaini ya wakuu wa Uturuki kuhusu kuboreka uhusiano wa pande mbili katika urais wa Donald Trump, hitilafu za nchi hizo mbili zinaonekana kushadidi.

Moja ya nukta muhimu za hitilafu baina ya Marekani na Uturuki ni sisitizo la wakuu wa Ankara kuhusu kununua mfumo wa makombora ya kujihami angani ya S-400 kutoka Urusi.

Disemba 2017, Uturuki na Urusi zilitiliana saini mapatano ya kununua mfumo huo wa S-400 na punde baada ya hapo Marekani ilianza kuwashinikiza wakuu wa Ankara wabatilishe mkataba huo. 

Hatua ya Uturuki ya kununua silaha hiyo muhimu ya  Urusi si tu kuwa ilipingwa vikali na Bunge la Marekani, Congress, na wizara ya ulinzi ya nchi hiyo, Pentagon, bali pia Washington imesonga mbele na kuchukua hatua za kivitendo kuizuia Uturuki kununu mfumo huo wa kujihami.

Uturuki ni mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Atlantiki ya Kaskaizni (NATO)  ambao unaongozwa na Marekani na unaoitazama Urusi  kama hasimu wake mkuu.

Kwa msingi huo Marekani imedai kuwa kuingiza mfumo wa S-400  katika mtandao wa kujihami angani wa nchi ya NATO ni jambo ambalo litapelekea Urusi  igundue siri za udhaifu wa ndege za kivita za nchi wanachama wa NATO hasa udhaifu wa ndege ya kivita ya Marekani ya kizazi cha tano ya F-35.

Aidha utawala wa Trump una wasiwasi kuwa iwapo Uturuki itanunua silaha za kistratijia za Russia, hatua kwa hatua nchi hiyo itajikurubisha zaidi kwa Moscow.

Pamoja na kuwepo mashinikizo hayo ya Marekani, lakini Uturuki inasisitiza kuwa itanunua mfumo huo wa makombora ya kujihami kutoka Russia.

 Mevlüt ÇavuÅŸoÄŸlu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki hivi karibuni aliashiria vitisho hivyo vya Marekani dhidi ya nchi yake na kusema: "Russia na Uturuki zimeshakamilisha mkataba wa mfumo wa S-400 wa makombora na hakuna yeyote anayeweza kuiambia Ankara ichague baina ya Magharibi na Russia."

Marekani imetupilia mbali sababu zilizotolewa na Uturuki kuhusu kununua mfumo wa S-400, na sasa inachukua hatua za kutaka kuilazimisha ibatilishe uamuzi wa kununua silaha hiyo.

Katika hatua ya kwanza, utawala wa Trump umekataa kuikabidhi Uturuki ndege za kizazi cha tano za F-35  mbali na kutoa vitisho vipya dhidi ya Ankara. 

Kwa mujibu wa mapatano, Marekani inapaswa kuikabidhi Uturuki ndege za kivita za F-35 mwaka huu wa 2019.

Marekani pia imetoa tishio la kuondolewa Uturuki katika muungano wa kijeshi wa NATO. 

Mike Pence, Naibu Rais wa Marekani akizungumza Aprili 3 aliitahadahrisha Uturuki kuhusu sisitizo lake la kununua makombora ya S-400 kutoka Russia na kusema: "Uturuki inapaswa kuchagua mawili, ima ibakie NATO au inunue S-400. Tishio hilo lilikabiliwa na jibu kali la wakuu wa Uturuki.

Katika tishio jipya dhidi ya Uturuki,  Robert Menendez  ambaye ni seneta wa ngazi za juu wa chama cha Democrats nchini Marekani amesisitiza kuwa, iwapo Uturuki itaendeleza mchakato wa kununua mfumo wa S-400 kutoka Russia, basi Marekani itaiwekea nchi hiyo vikwazo na haitaikabidhi ndege za kivita za F-35.

Kwa mtazamo wake, hatua ya Uturuki ya kununua S-400 ni sawa na kununua zana muhimu ya kijeshi kutoka Russia na jambo hilo litapelekea Ankara ikumbwe na vikwazo vya Marekani. Amesema nchi yoyote itakayonunua silaha kama hiyo ya Russia pia itawekewa vikwazo.

Mendez amesisitiza kuwa: "Hatuwezi kuweka ndege ya kivita ya F-35 pembeni mwa mfumo wa makombora wa S-400 kwani jambo hilo litapelekea siri za F-35 kugundulika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com