Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHUNGAJI AKEMEA RUSHWA NA WANASIASA WANAOVURUGA AMANI


Mchungaji Kiongozi wa kanisa la Shekinah Presbyterian lililoko Madale, jijini Dar es salaam Mch. Daniel John Seni amekemea vikali vitendo vya baadhi ya viongozi kuwaaminisha uongo watu wengine kwa manufaa yao binafsi. 

Akihubiri katika ibada ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka kwa mwaka 2019 alidai kuwa “watu waliokuwa wakipiga kelele kwamba Yesu asulubiwe waliaminishwa kwamba Yesu ni mtu mbaya na hafai, na ndiyo maana walianza kupiga kelele kwamba “na asulubiwe”. Lakini ukweli ni kwamba wale wakuu wa makuhani waliwashawishi makutano kwa ajili ya kutetea maslahi yao ambayo yalikuwa yanahatarishwa na Yesu ambaye aliwaambia ukweli mkavu kwa matendo waliyokuwa wakifanya. 

Aliendelea kusema kwamba “hivi wanasiasa wengi wamekuwa wakiwatumia watu wasiojua chochote kuandamana pasipo hata kujua kwa nini wanaandamana!” Watenda mema katika jamii yetu wameanza kuonekana ni wabaya kwa sababu ya nguvu ya ushawishi ya watenda mabaya, ni lazima mambo haya tuyakemee katika jamii zetu. Ni jukumu letu kuhakikisha kwamba tunapata ukweli katika kila jambo, ili tusije tukadanganywa kwa kuaminishwa kwamba fulani ni mbaya kumbe sivyo.


Vile vile aliongelea kitendo cha Wakuu wa Makuhani kujaribu kuuaminisha umma kwamba Yesu Kristo hakufufuka kutoka wafu. 

Alielezea kuwa “Wakuu wa Makuhani baada ya kuona kwamba ushawishi wao wa kwanza umegonga mwamba, waligeukia upande wa pili kwa kuwahonga askari wao ili kuuaminisha umma maneno ya uongo. 

Hata hivyo alikemea vikali vitendo vya rushwa katika jamii kwa madai kwamba “kitendo cha wale askari waliokuwa wakilinda kaburi la Yesu kukubali kupokea rushwa ili kufunika ukweli kilikuwa ni kitendo cha aibu sana kwao. 

Askari hawa waliamua kuisaliti kazi yao kwa kudanganya kwamba walikuwa wamelala! Ni mlinzi gani anayeweza kusema kwamba nimeibiwa kwa sababu nilikuwa nimelala? Kazi ya askari ni kazi inayohitaji uaminifu mkubwa lakini hawa askari walijishushia heshima kwa kupokea kitita cha pesa ili wazibwa midomo yao.


Akiwageukia watu wanaopenda kutoa rushwa ili kuziba ukweli kwa faida yao binafsi mchungaji huyu alisema kuwa “ni jambo la aibu kwa viongozi kutoa rushwa ili kuziba midomo ya watu, tunajua kwamba rushwa huziba ukweli na hupotosha macho ya watu.” 

Aliongeza kwamba” tumekaribia kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa, watu wa Mungu kataeni rushwa, kataeni kufunikwa macho yenu, msikubali kuchagua viongozi ambao hawafai eti kwa kisingizio cha kwamba amekupa chochote.”


Mchungaji huyu aliendelea kusema kwamba “katika maisha yetu ya kila siku tunahitaji kutumia pesa, lakini lazima tujue kwamba pesa tuliyo nayo imepatikana kwa njia gani? Askari hawa alipata pesa kubwa kwa ajili ya kufunika ukweli kwamba Yesu Kristo alifufuka kutoka kwa wafu. 

Inawezekana katika jamii zao walianza kuheshimiwa kwa kuwa na pesa, lakini je pesa hizo zilikuwa ni pesa halali? Epuka pesa ya rushwa na acha kutoa rushwa, ni lazima tuwe wakweli ili nchi yetu iendelee mbele.


Ibada hii ilijumuisha kushiriki Meza ya Bwana, tendo ambalo Bwana Yesu aliliagiza kwa wanafunzi wake kwamba wafanya hivyo kwa ajili ya kukumbuka mateso yake, na ni tendo ambalo hupokelewa kwa Imani na Wakristo ulimwenguni.
HERI YA PASAKA, 2019
________________________
Imetolewa na ofisi ya Mchungaji,
Shekinah Presbyterian Church Tanzania
0769080629 au spctanzania@gmail.com


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com