Hospitali moja katika Kaunti ya Machakos nchini Kenya imeingia matatizoni baada ya kupotea kwa kichanga ambacho kimezaliwa hapo, na mama aliyekwenda kujifungua.
Ndugu wa mwanamke ambaye amepotelewa na mtoto wamesema kwamba waliambiwa na wauguzi kuwa mtoto alifariki, lakini mpaka sasa hawajakabidhiwa mwili wake kama inavyotakiwa.
“Dada yangu alijifungua kwa upasuaji, akawataka waoneshwe mwili wa mtoto wake, lakini mpaka sasa uongozi wa hospitali umeshindwa kufanya hivyo, badala yake wanatuzungusha tu”, amesema mmoja wa ndugu hao.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Afya wa Kaunti ya Machako Dr. Joel Mwova amesema kwamba tukio hilo ni kwlei limemfikia mezani kwake na lipo kwenye uchunguzi.
“Nilipewa namba ya mmoja wa ndugu, nikampigia na kuambiwa kuwa yuko kwenye kikao na wakuu wa idara nyingine, nataka nipate ripoti kutoka kwa kiongozi wa wauguzi, ndipo nitoe ripoti yangu”, amesema Dr. Mwova.
Mkurugenzi huyo ameongeza kwamba iwapo ikithibitika upotevu wa mtoto huyo hilo ni kosa la jinai, ambalo sheria itatakiwa ifuatwe kwa wahusika.