Wakazi wa kijiji cha Nakapyata, wilayani Buyende nchini Uganda wamefanya sherehe ambapo watoto wawili walio kati ya umri wa miaka tisa na sita waliozwa katika utamaduni wa kushangaza.
Kulingana na mtandao wa gazeti la Daily Monitor nchini Uganda Uganda, mvulana huyo ambaye yuko katika darasa la nne katika shule ya msingi ya Buyende na msichana ambao wote waliripotiwa kuzaliwa na meno mawili waliozwa siku ya Jumatatu na kupatiwa nyumba ya kitamaduni kuishi.
Chini ya sheria za Uganda , ni makosa kwa watu walio chini ya umri wa miaka 18 kufunga ndoa ama hata kushiriki katika tendo la ngono.
Inadaiwa kuwa watoto hao wawili walianza kuchumbiana wakati mvulana alipokuwa na miaka mitatu na msichana akiwa na umri wa miezi mitatu pekee.
Hatua hiyo baadaye iliimarisha uhusiano kati ya familia zote mbili , huku Delifazi Mulame babake mvulana akimuita msichana huyo kama 'mke wa mwanangu'.
''Mwanangu alizaliwa na meno mawili na mkewe akazaliwa na meno mawili. Kuzaliwa kwake kulileta baraka nyingi na jina lake linapaswa kuwaunganisha watu wa makabila ya baganda na basoga'', alisema bwana Mulame.
Bi Barbra Namulesa , mwalimu wa mvulana huyo alimtaja kuwa mwenye nidhamu , mtu wa watu anayezungumza kama mzee wa kijiji.
''Nadhani hii ndio Kintu ambayo wazee wetu walizungumzia. Yeye hunishauri licha ya mimi kuwa mwalimu wake'',alisema.
Bi Mwadi Mutesi, mwenye umri wa miaka 38, ambaye ndiye mamake msichana anasema mwanawe amekuwa mtu wa kushangaza tangu alipozaliwa.
''Alianza kuzungumza mara tu baada ya kuzaliwa , wakati nilipokuwa na uchungu wa kujifungua niliuliza ni mtoto wa jinsia gani na nikaambiwa ni msichana''.
''Hatahivyo mkunga alinishangaza wakati aliposema kuwa mwanangu amezaliwa na meno mawili. karibu nimuangushe, mamake aliye na watoto saba alisema.
Aliongezea: Hofu yangu ilikuwa kumnyonyesha mtoto mwenye meno.
Chanzo - BBC
Social Plugin