Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Makampuni ya Simu nchini, itawezesha zoezi la uandikishaji wa watumiaji wa simu nchini kwa kutumia Namba za Utambulisho wa Taifa au Kitambulisho cha Taifa.
Zoezi la Uandikishaji wa laini za simu linatarajia kufanyika kuanzia tarehe 01-Mei-2019. Mazoezi ya majaribio ya zoezi hili yamefanyika katika baadhi ya Mikoa na Taasisi na kuonyesha mafanikio.
NIDA tayari imesajili asilimia 88 ya watu wote wanaostahili kusajiliwa kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa nchi nzima.
Zoezi la Utambuzi na usajili ni endelevu, hivyo asilimia 12 ya lengo la usajili lililobaki linaendelea kutekelezwa katika wilaya zote nchini kwa kusajili watu ambao hawakusajiliwa kwenye zoezi la usajili wa umma (Mass Registration) na ambao wamekisha umri wa miaka 18, ambacho ni kigezo cha kisheria kinachoruhusu mwananchi kusajiliwa kwa ajili ya Utambulisho wa Taifa.
Vile vile usajili wa umma unafanywa tena katika mikoa ambayo watu wengi hawakusajiliwa katika usajili wa awali. Mikoa hiyo ni pamoja na Dar es salaam, Tanga, Pwani na Kigoma.
NIDA tayari imetengeneza Namba za Utambulisho wa Taifa Milioni 12, sawa na asilimia na 59 ya usajili uliofanyika. Zoezi la uhakiki, kuchakata na kutengeneza Namba za Utambulisho wa Taifa linaendelea kutekelezwa kwa kasi usiku na mchana.
Aidha tunatoa rai kwa wale wote ambao wamejulishwa kuwa vitambulisho vyao vipo tayari wafike Ofisi za NIDA au Ofisi za Serikali za Mitaa walipo jiandikishia kuvichukua. Vitambulisho vya Taifa vinaendelea kuzalishwa na kusambazwa kwa wananchi. Namba za Utambulisho wa Taifa zitatumika katika usajili wa Namba za simu na matumizi mengine. Hivyo wale ambao tayari wana Namba za Utambulisho wa Taifa wazitumie kujisajili wakati vitambulisho vinazalishwa.
Wananchi mnaweza kupata Namba ya Utambulisho wa Taifa na huduma zingine zitolewazo na NIDA kwa njia zifuatazo:-
a. Kupiga namba * 152 *00#; chagua Ajira na Utambuzi; Chagua NIDA
b. Kupakua nakala ya Kitambulisho cha Taifa kwa kutembelea tovuti: http://bit.ly/2VuiGwR au tovuti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa.
c. Kupiga simu huduma wateja; 0673 333444, 0743 202020, 0743 201020,
d. 0759 102010, 0765 201020.
e. Kufika ofisi za NIDA ya Wilaya ilyopo karibu.
Ni Muhimu kwa Wananchi wote wenye sifa za kusajiliwa kwa ajili ya Utambulisho wa Taifa kufanya hivyo sasa pasipo kusubiri mpaka wanapokuwa na hitaji la haraka kwani uhakiki wa taarifa zako lazima ufanyike kabla ya utoaji wa Namba ya Utambulisho wa Taifa na baadae kitambulisho cha Taifa.
“Utambulisho wa Taifa kwa Maendeleo na Ustawi wa Nchi Yetu”
Imetolewa na
MAMLAKA YA VITAMBULISHO VYA TAIFA
23 APRILI, 2019.
Social Plugin