Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akizungumza kwenye kikao cha mrejesho wa kazi za viongozi wa jamii kata ya Usanda katika kutokomeza mila na desturi kandamizi katika jamii - Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Imeelezwa kuwa migogoro ya wanandoa imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa watoto kukosa haki zao matokeo yake wanafanyiwa vitendo vya kikatili.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 16,2019 na Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo kwenye kikao cha mrejesho wa majukumu ya viongozi wa jamii kata ya Usanda katika kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kikao hicho kimeandaliwa na Shirika la Agape ACP ambalo linalenga kutokomeza mila na desturi kandamizi zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kupunguza mimba na ndoa za utotoni na maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Afisa ustawi huyo wa jamii aliwataka wanandoa kuvumiliana panapotokea migongano kwani hakuna ndoa takatifu huku akibainisha kuwa pale wanandoa wanapoachana wanaoteseka zaidi huwa ni watoto.
“Wanaume mmekuwa na kasumba na kuuza mazao na kuamua kuoa wanawake wengine matokeo yake mnaacha watoto wakiteseka,mnasahau hadi majukumu ya kuwalea na kuwasomesha matokeo yake watoto hawa wanaanza kuiga tabia za makundi mabaya”,alisema Mweyo.
“Mtoto anahitaji mapenzi ya baba na mama,ndoa inaposambaratika watoto wanakosa pa kwenda,wengine wanaamua kuacha hata kwenda shule na kujiunga kwenye makundi yasiyofaa,mbaya zaidi wanaume wakipata mke mpya wa kwanza anamsahau,anasahau hadi kuwapatia haki watoto wake”,alieleza Mweyo.
Aidha aliwashauri wananchi kuwa mstari wa mbele kubadilisha mila na desturi zisizofaa katika jamii ikiwemo kurithi wajane, kuozesha watoto na kutopeleka watoto shule akieleza kuwa mabadiliko yataletwa na wao wenyewe.
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape unaofadhiliwa na shirika la Sida la nchini Sweden, Lucy Maganga aliwaomba viongozi wa jamii kufanya kazi ya kutokomeza mila na desturi kandamizi kwa weledi ili kuondoa ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Kwa upande wao,viongozi hao wa jamii walilishukuru shirika la Agape kwa kuwafikia na kuwapatia elimu ya kukabiliana mila na desturi kandamizi huku wakisema hivi sasa jamii ya Usanda imebadilika na matukio ya mimba na ndoa za utotoni yamepungua.
“Tumeendelea kutoa elimu kwa jamii,kwa kweli mwitikio umekuwa mzuri ,na sasa ile kasumba ya kwamba baba ndiyo kila kitu katika familia imeisha”,alisema Juma Katabuka kutoka Shabuluba.
“Hivi sasa jamii imeanza kuacha tabia ya kurithi wajane kwani imeshatambua madhara yake kwani huko ni kumfanyia ukatili mwanamke lakini pia ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya zinaa ukiwemo UKIMWI,kwani huwezi kujua marehemu alifariki kwa ugonjwa gani”,alisema Ramadhan Kulwa ambaye ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwagala.
Naye Singu Njegi kutoka kitongoji cha Munge alisema kutokana na elimu waliyopata wataendelea kuzifikia kaya na makundi mbalimbali ili kila mtu atambue mila na desturi kandamizi zinachangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa Mtendaji wa kata Usanda Emmanuel Maduhu akizungumza wakati wa kikao cha mrejesho wa kazi zilizofanywa na viongozi wa jamii kata ya Usanda kilichofanyika leo katika shule ya msingi Shingida. Maduhu alisema Shirika la Agape limesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua mimba na ndoa za utotoni katika eneo hilo- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape Lucy Maganga akiwahamasisha viongozi wa jamii kuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za watoto na wanawake ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa mila na desturi kandamizi katika jamii.
Viongozi wa jamii wakiwemo viongozi wa kimila na Wazee maarufu kata ya Usanda wakimsikiliza afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape Lucy Maganga.
Afisa mradi wa afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape Lucy Maganga akizungumza wakati wa kikao hicho.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akiwataka viongozi wa jamii kuwakumbusha wanandoa kuvumiliana ili familia zisitawi vizuri kwa maslahi ya kulinda haki za watoto kwani ndoa zinaposambaratika watoto wengi hukosa mwelekeo wa maisha matokeo yake wanajiingiza kwenye makundi yasiyofaa.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Elizabeth Mweyo akizungumza katika kikao hicho.
Mzee Singu Njegi kutoka kitongoji cha Munge akitoa mrejesho wa kazi anazofanya kutokomeza mila na desturi kandamizi katika jamii.
Kaimu Mwenyekiti wa kitongoji cha Kanyenye,Daudi Michael akielezea namna anavyohamasisha wazazi kupeleka watoto shule.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Nzega kijiji cha Shigita,Mwinyi Albinus akielezea namna anavyoendelea kuielimisha jamii kuachana na mila na desturi kandamizi zinazochangia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kikao kinaendelea.
Mwakilishi wa kundi la watu wenye ulemavu Mayunga Mayunga akielezea jinsi anavyotoa elimu kwa jamii kuachana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Washiriki wa kikao hicho wakiwa ukumbini.
Mwakilishi wa kundi la vijana,Suzana Amos kutoka kitongoji cha Munge akielezea jinsi anavyotoa elimu kwenye kaya mbalimbali kuhusu madhara ya mila na desturi kandamizi.
Simon Makenza kutoka Nzagaluba akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Muelimisha rika kata ya Usanda,Hamis Malundi akichangia hoja wakati wa kikao hicho.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwagala, Ramadhan Kulwa akizungumza wakati wa kikao hicho.
Ng'wanzalima Malimi kutoka kitongoji cha Buchamike akizungumza wakati wa kikao hicho cha viongozi wa jamii.
Afisa Ustawi wa Jamii kata ya Usanda, Halima Tendeja akifunga kikao cha mrejesho wa kazi za viongozi wa jamii katika kutokomeza mila na desturi kandamizi. Tendeja alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wanaume kushauriana na wenza wao kupanga uzazi kwani bado baadhi ya wanawake wamekuwa wakiogopa kupanga uzazi kwa kuogopa waume zao.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin