Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limezuia mkutano wa ndani wa Kiongozi wa Chama wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe wa uzinduzi wa matawi kutokana na kuwapo vurugu.
Hatua hiyo ilitokana na taarifa za intelijensia ambazo zilidai kutokea vurugu ambazo ziliratibiwa na wanachama na wafuasi wa Chama cha CUF.
Akizungumza hali hiyo jana, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola vya kuzuia shughuli za chama hicho vinaonyesha namna ambavyo kinahofiwa kwa kuwa na nguvu kubwa kwa umma.
Alisema zuio hilo linaonyesha namna wanavyoingizwa kwenye mitego ya wanachama wao waonekane wanafanya vurugu.
Ziito alidai kumekuwa na mazuio ya kila mara kwa chama hicho kinapojaribu kufanya shughuli zake kama vile mikutano ya ndani ya kuimarisha uhai wa chama .
Hata hivyo kiongozi huyo alishangazwa na jeshi hilo kuruhusu vyama vingine kama CUF na CCM kuendelea kufanya mikutano ya ndani na hadhara bila ya vizuizi vya aina yoyote ile.
Alisema mpaka jana Jeshi la Polisi Wilaya ya Tanga, lilikuwa limetoa kibali kwa chama hicho kuendelea kufanya shughuli zake ikiwamo kupokea wanachama wapya na mikutano ya ndani kabla ya kuzuia shughuli hizo.
Akizungumzia hali zuio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe, alisema taarifa za intelejensia zinaonyesha iwapo chama hicho kitaruhusiwa kufanya shughuli zake kunaweza kutokea uvunjifu wa amani.
Alisema kutokana na uchunguzi wao walibaini baada ya kuwapo mivutano ya siasa baina ya chama hicho na CUF kutokana na kunyang’anyana ofisi na kuharibu baadhi ya thamani za ofisi hizo jambo linaloweza kusababisha kutokea vurugu na amani kutoweka.