Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwili wa aliyekuwa Ofisa wa Wizara ya Madini, Mery Mkwaya Maramo (35), aliyefariki mwanzoni mwa wiki hii na kuzikwa jana katika makaburi ya Pugu-Mwakanga jijini Dar es Salaam, umefukuliwa na kutolewa nje ya jeneza kisha kuvuliwa nguo usiku wa kuamkia leo, Ijumaa, Aprili 12, 2019 na watu wasiojulikana.
Kaka wa marehemu Mary aitwaye Deogratius Maramo, amedai mwili wa marehemu uliingiliwa kimwili na kueleza kuwa bado wanasubiri ripoti ya polisi ili kujua kilichotokea kwani hakuna kitu chochote kilichoibiwa katika kaburi hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Ilala, Zuberi Chembela akizungumzia tukio hilo amesema tukio hilo lilitokea leo saa 1:00 asubuhi katika makaburi ya Pugu Mwakanga ambapo mwili huo wa marehemu pia ulikutwa umevuliwa nguo.
Amesema taarifa za kufukuliwa mwili huo zilitolewa na fundi aliyejenga kaburi hilo ambaye alieleza alienda kwa ajili ya kumwagilia ndipo aliukuta ukiwa umevuliwa nguo huku nusu ukiwa nje na nusu ukiwa ndani ya kaburi.
“Huyu marehemu alifariki Aprili 8 mwaka huu mkoani Dodoma na alizikwa jana ambapo leo tulipata taarifa baada ya fundi aliyejenga kaburi kutoa taarifa katika kituo cha polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga ndipo askari polisi walienda kwenye tukio na kukuta kaburi limevunjwa huku mwili wa marehemu ukiwa umevuliwa nguo” amesema.
Kamanda Chembera amesema baada ya maofisa wa polisi kufika katika tukio hilo walifanya mahojiano na ndugu wa marehemu hivyo walikubaliana kuurudisha mwili kaburini na kuujengea tena.
Amesema tukio hilo ni la kijinai hivyo wanaendelea kulichunguza na watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, amesema wao hawawezi kuthibitisha kama mwili wa marehemu umeingiliwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu kwa kuwa taratibu za uchunguzi zinatakiwa itolewe kibali na Mahakama ili daktari aufanyie uchunguzi.
Amesema jeshi la polisi lipo tayari kushirikiana na ndugu wa marehemu endapo watafuata taratibu za kisheria watakazoambiwa.
Social Plugin