Chama Cha Wananchi (CUF) kimewateuwa wanachama 13 kushika nafasi mbalimbali za uongozi ili kusaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, aliwaeleza waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, wameteua wanachama ambao miongoni mwao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Wanachama walioteuliwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Zainab Mndolwa na naibu wake, Omar Mohammed Omar, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera, Mohammed Habibu Mnyaa na naibu wake, Mohammed Ngulangwa.
Wengine ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar na naibu wake, Mohammed Vuai Makame, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Abdul Kambaya na naibu wake, Mbarouk Seif Salim.
Wengine ni Haroub Mohammed Shamis aliyeteuliwa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, naibu wake Salvatory Magafu wakati Thinney Juma Mohammed akiteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mafunzo na Uhamasishaji na naibu wake, Masoud Omary Mhina.
Profesa Lipumba alisema Kamati ya Uongozi imemteua Yusuph Mohammed Mbugiro kuwa Ofisa Tawala wa ofisi kuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo wa CUF pia amefanya uteuzi wa viongozi wa jumuiya za chama huku akisema viongozi hao watakaimu nafasi zao mpaka pale watakapochaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali ameteuliwa kuwa kaimu mwenyekiti Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), makamu wake Faki Suleiman Khatib na kaimu Katibu Mtendaji, Yusuph Kaiza Makame na naibu wake, Mbaraka Chilumba.
Kaimu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake (Jukecuf) ni Dhifaa Mohammed Bakar na makamu wake ni Kiza Mayeye, kaimu Katibu Mtendaji ni Anna Ryoba na naibu wake ni Leila Jabir Haji.
Kwa upande wa Jumuiya ya Wazee wa Cuf (Juzecuf), kaimu mwenyekiti ni Mzee Chunga na makamu wake ni Hamida Abdallah, kaimu katibu mtendaji ni Hamis Makapa na naibu wake ni Said Ali Salim.
Social Plugin