Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayoongozwa na Seleman Jafo kuhamia katika jengo la ofisi yao ‘pagale’ ambayo haijakamilika hivyo hivyo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana ikiwa ni muda mfupi baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kueleza kuwa alikuwa na makubaliano na mawaziri kuwa siku majengo hayo yakizinduliwa mawaziri wangehamia.
Hata hivyo, Majaliwa alimweleza Rais kuwa kuna baadhi ya wizara ikiwemo Tamisemi ambazo majengo yao yamechelewa kukamilika kutokana na kuchelewa kupata fedha.
Waziri Mkuu alitaja muda ambao majengo hayo yatakamilika ni mwishoni mwa Aprili huku jengo la Tamisemi likielezwa litakuwa tayari mwishoni mwa Mei kutokana na ramani yake kuwa tofauti na majengo mengine.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema hataki kusikia kunakuwa na kisingizio cha majengo mengine kuwa hayajakamilika na badala yake kama mtu ameshindwa basi akae hata chini ya mwembe ili mradi awe Mtumba ambako ndiko mji wa kiserikali uliko.
Kiongozi huyo alisema muda wote atakapokuwa anawahitaji mawaziri, hakuna sababu ya kuwaita bali atawafuata kwenye majengo hayo hivyo akaomba kila mmoja wao ahamie kwa vitendo siyo maneno.
Social Plugin