Rais John Magufuli amewajia juu wakandarasi wasiofanya kazi zao vizuri na kwa wakati na kuitaka Wizara ya Ujenzi kuwachukulia hatua za kisheria ikibidi wafukuzwe kazi kwani wameifanya Tanzania ni nchi ya majaribio.
Ametoa kauli hiyo leo jumatano Aprili 3, wakati akizungumza na wananchi katika ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Mtwara ambapo ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Barabara kutoka Mtwara -Newala – Masasi yenye urefu wa kilomita 210.
“Wakandarasi mliosajiliwa katika nchi hii mbadilike na wizara muendelee kutumia sheria namba 17 ya mwaka 1997 na wale wasiofanya kazi vizuri wafukuzwe Tanzania isiwe nchi ya majaribio, Oktoba nitatenga muda kuja kuangalia kama huu mradi umekamilika na ole wenu nikute haujakamilika tutazungumza lugha nyingine.
“Tunataka lami na nikuombe Waziri pamoja na kazi nzuri mnayoifanya katika bajeti ya mwaka huu muhakikishe mnatangaza kilomita nyingine 50 kwenda mbele na mwaka mwingine tena 50 au 100 itategemeana fedha tutakazokuwa nazo,” amesema
Aidha amewataka wananchi wa Mtwara kudumisha amani na mshikamamo kati yao na kuachana na tabia ya kubaguana ili waweze kusaidiana kukuza uchumi wa nchi kwa kufanya kazi kwa pamoja.
“Tukishakuwa na miundombinu mizuri, umeme na maji Mtwara patakuwa ni mahali ambapo kila mtu atataka kupakimbilia endeleeni kuwa na mshikamano msibagueni kwaajili ya vyama wala dini mimi ni rais wa wote lengo ni kupeleka maendeleo ya nchi mbele,” amesema