Na Mwandishi Wetu,MAELEZO
Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa siku 30 kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kukamilisha ujenzi wa stendi Kuu ya Mabasi katika Mkoa wa Njombe ambayo ujenzi wake imechukua muda wa miaka 5 bila kukamilika.
Akizungumza katika Mkutano wa hadhara na Wananchi Mkoani humo leo Jumatano (April 10, 2019), Rais Magufuli alisema mradi huo ni haki ya wananchi kutokana na tozo ya kodi mbalimbali wanazokatwa hivyo anashangwa na kitendo cha stendi hiyo kutokamilika licha ya mkandarasi wa mradi huo kulipwa fedha zote na Serikali.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema Serikali haipo tayari kuwavumilia wakandarasi wazembe na kutoa maelekezo kwa mkandarasi wa awali wa mradi huo ambayo ni kampuni ya Masasi Construction kuchunguzwa haraka na iwapo atabainika na makosa achukuliwe haraka hatua kali kwa mujibu wa sheria.
Aliongeza kuwa katika Serikali anayoiongoza hatoruhusu viongozi na watendaji wabaishaji na badala yake aliwaomba kuwajibika katika maeneo yao bila ya kufuatwa na Rais kwa kuwa majukumu aliyonayo ni mengi hivyo kuwataka kuwatumikia wananchi kwani wamechelewesha maendeleo yao kwa kipindi kirefu.
“Ipo miradi mingi ambayo imechelewa kwa kipindi kirefu tu ukiwemo huu wa stendi ya Mabasi katika Mkoa wa Njombe, tumechezewa vya kutosha na nyingi Viongozi na watendaji nawaagiza uamuzi usisubiri Rais mpya nina wawakilishi wangu ambao ni nyinyi timizeni wajibu wenu” alisema Rais Magufuli.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema anashangwa na mradi huo uliogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 9 kushindwa kukamilika kwa wakati huku baadhi ya miradi kama hiyo ikitekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini, hivyo kitendo kilichofanywa na mkandarasi wa mradi huo ni cha ubabaishaji na kupongeza hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa kwa kusimamisha haraka ujenzi wa stendi hiyo.
Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kutimiza ahadi zote ilizoahidi kwa wananchi wake, na hivyo hawatakubali kuona Mtendaji au Kiongozi yoyote anakwamisha jitihada hizo, kwani hayupo tayari kusema uongo mbele ya wananchi kwa kuwa ni dhambi.
Aliongeza kuwa katika mradi wa Stendi hiyo Serikali imetumia kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni fedha za wananchi maskini na hivyo aliitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuwa thamani halisi ya fedha ya mradi huo inapatikana na mradi huo unakamilika kwa muda na wakati uliopangwa.
Akitoa taarifa ya Mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe Mji, Bi Illuminata Mwenda alisema mradi huo unaotekelezwa kwa ujenzi awamu tatu ulianza mwaka 2013, ambapo mkandarasi wa kampuni ya Masasi Construction amelipwa fedha zote na Serikali lakini halmashauri hiyo imesitisha mkataba wake kutokana mkandarasi huyo kushindwa kuikamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Awali akitoa taarifa ya hali ya Maji katika Mkoa wa Njombe kwa Rais Magufuli, Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa alisema Serikali imeongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika Mkoa huo kutoka asilimia 39 mwaka 2015 hadi asilimia 67 kwa sasa, hatua iliyotokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji katika miji ya Njombe Mji na Njombe Mjini wenye wenye gharama ya Tsh Bilioni 12.5
Aidha alisema pamoja na mradi huo, Serikali pia imepata ufadhili kutoka Serikali ya India kupitia mradi wa maji utakaotekelezwa katika miji 28 nchini ikiwemo mji wa Njombe na Njombe wenye gharama ya Tsh Bilioni 32 ambao mwezi Septemba mwaka huu mkandarasi anatarajiwa kukamilisha nyaraka mbalimbali za zabuni.
Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Serikali imeendelea kuimarisha na kuboresha utoaji wa huduma ya afya Mkoani Njombe ikiwemo Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo ambayo ujenzi umegharimu kiasi cha Tsh Bilioni 3.5.
Aliongeza kuwa katika kuimarisha mfumo wa utoaji huduma katika hospitali hiyo ambapo Serikali imepanga kuiwezesha hospitali hiyo vifaa tiba na wataalamu wakiwemo Madaktari Bingwa wa magonjwa yote yakiwemo ya uzazi, upasuaji na mipasuko ya ajali.
Alisema hadi kufikia sasa Serikali inasomesha jumla ya Madaktari Bingwa 301 katia vyuo mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa hospitali, vituo vya afya na Zahanati zote nchini zinakuwa na watalaamu wa kutosha na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto.
Social Plugin