Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameendelea na ziara yake katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ambapo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya lami ya Mbinga – Mbambabay na kuzungumza na wananchi.
Ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay yenye urefu wa kilometa 67 utagharimu shilingi Bilioni 134 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Tanzania na unakamilisha barabara nzima ya ushoroba wa maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) yenye urefu wa kilometa 1,020.
Kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Masumuni Mjini Mbinga, Rais Magufuli amewaongoza wananchi kusimama kwa dakika 1 kumkumbuka na kumuombea Hayati Abeid Amani Karume ambapo jana ni kumbukumbu ya siku ya kifo chake.
Rais Magufuli ameishukuru AfDB kwa kutoa mkopo wa ujenzi wa barabara hiyo na amemtaka mkandarasi anatekeleza kazi hiyo (China Henan Internatinal Cooperation Group Co. Ltd – CHICO) kukamilisha ujenzi kabla ya kuisha kwa mwaka 2020 badala ya mwaka 2021 kama ilivyopangwa.
Amewapongeza wananchi wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kufanikisha ndoto ya kukamilishwa kwa barabara ya kuanzia bandari ya Mtwara hadi bandari ya Mbambabay na kubainisha kuwa itaongeza fursa za uchumi kwa wananchi na Taifa ikiwemo kuwahakikishia soko la ndani na nje ya nchi kwa mazao ya wakulima.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli amejibu kero za wananchi zilizotolewa na Mbunge wa Mbinga Mjini Sixtus Mapunda kwa kuagiza vyombo vya dola kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kuifilisi Benki ya Wananchi wa Mbinga ambayo ilikuwa ikiwasaidia wananchi hasa wakulima.
Rais Magufuli amewataka viongozi wa wilaya ya Mbinga wakiwemo Wabunge kuwafichua watu waliohusika kuwadhulumu wakulima wa kahawa katika msimu uliopita ili Serikali ichukue hatua.
Aidha, amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga kwa hatua zinazochukuliwa na wizara yake kuanzisha mnada wa kahawa Wilayani Mbinga, hatua ambayo itawasaidia wakulima kupata soko la uhakika na kuepusha dhuluma na wizi.
“Nataka niwahakikishie ndugu zangu kuwa katika awamu yangu mafisadi hawatapenya, tumefanikiwa kuondoa watumishi hewa, kaya masikini hewa zilizokuwa zinapewa fedha za TASAF na tutaendelea kusimamia nidhamu ya kazi na kusimamia kila senti ya Serikali” Rais Magufuli.
Rais Magufuli amezungumzia zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali ambapo amewaonya viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao hawagawi vitambulisho hivyo licha ya wananchi kuvihitaji na pia ametaka viongozi hao wasiwalazimishe watu kuvinunua.
“Viongozi wa Mikoa na Wilaya ambao hamgawi vitambulisho maana yake mnapingana na maelekezo yangu, na ndugu zangu wajasiriamali ambao hamfanyi juhudi za kupata vitambulisho hivyo najua itafika siku wale ambao hawana vitambulisho watazuiwa kufanya biashara, ikifika hapo sitawatetea” amesisitiza Rais Magufuli.