Ripoti ya kurasa 448 kuhusu uchunguzi maalum kubaini iwapo Urusi iliingia Uchaguzi wa urais nchini Marekani mwaka 2016 imewekwa wazi baada ya uchunguzi wa miaka miwili kumalizika.
Uchunguzi huo uliongozwa na Robert Mueller aliyewahi kuwa mkuu wa FBI na imebaini kuwa ni kweli Urusi ilijaribu kuingilia Uchaguzi huo.
Hata hivyo, katika ripoti hiyo, haikubainika iwapo kampeni ya rais wa sasa Donald Trump ilishirikiana na Urusi au raia yeyote wa Marekani.
'Baada ya uchunguzi wa miaka miwili, maelfu ya watu kujitokeza na mamia kutoa ushahidi, imebainika kuwa ni kweli Urusi ilijaribu kuingilia Uchaguzi wa Marekani lakini wale waliomsaidia Trump kufanya kampeni hawakuhusika," amesema Mwanasheria Mkuu William Barr.
Mawakili wa Trump wamesema kuwa ripoti hiyo ni ushindi mkubwa kwa upande wao baada ya kushtumiwa hapo awali kuwa, Trump alisaidiwa na Urusi kuingia madarakani.
Pamoja na hilo, ripoti hiyo imeeleza kuwa rais Trump alijaribu kushawishi kufutwa kazi kwa Mueller aliyekuwa anaongoza uchunguzi huo.
Trump amekuwa akisema kuwa hakuwahi kushirikiana na Urusi, kushinda Uchaguzi wa mwaka 2016.
Social Plugin