Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ripoti ya CAG: MAPUNGUFU YALIYOBAINIKA KATIKA UKAGUZI WA VYAMA VYA SIASA

==>>Yafuatayo ni baadhi ya mambo yaliyobainika katika ukaguzi wa Vyama vya Siasa.
(a) Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilinunua gari jipya aina ya Nissan Patrol kwa Dola za Marekani 63,720 (sawa na shilingi milioni 147.76) ambalo lilisajiliwa kwa jina la mwanachama badala ya jina la Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA. 

Pia, gari hilo  lilioneshwa kwenye taarifa za fedha kama mkopo kwa mwanachama huyo bila kuwa na makubaliano ya mkopo yaliyosainiwa kati ya mwanachama na Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA.
(b) Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakikuwasilisha michango ya kila mwezi kwenda Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hadi kufikia Mei, 2018 chama hicho kilikuwa na deni la shilingi bilioni 3.74 ambalo linajumuisha adhabu ya shilingi bilioni 2.73 iliyotokana na ucheleweshwaji wa uwasilishaji wa michango hiyo.
(c) Aidha, nilibaini kuwapo kwa tatizo la uendelevu wa biashara (Going concern) katika Kampuni ya Uchapishaji ya Uhuru inayomilikiwa na CCM. Pia, hati za ardhi za nyumba 199 zinazomilikiwa na CCM Zanzibar zilionekana hazijasajiliwa kwa jina la Bodi ya Wadhamini bali zimesajiliwa kwa majina ya maofisa wa Chama.
(d) Vyama saba vilifanya matumizi ya jumla ya shilingi milioni 777.91 bila ya kuwa na nyaraka toshelevu na hivyo nilishindwa kuthibitisha iwapo malipo hayo yalikuwa halali; na iwapo yalihusiana na shughuli za vyama hivyo. Vyama hivyo vimeainishwa katika Jedwali Na. 11
==>Mapendekezo kwa Serikali Kuu na Vyama vya Siasa
Ili kurekebisha kasoro nilizozibainisha, ninashauri yafuatayo:
(i) Serikali ifanye juhudi za makusudi kuziwezesha Mamlaka za Rufaa za Kodi ili kuhakikisha mashauri ya kodi yanashughulikiwa kwa wakati ili kupunguza mrundikano wa mashauri.


(ii) Serikali idhibiti mifumo ya ukusanyaji wa tozo za huduma za usafiri kwenye viwanja vya ndege na bandari. Pia, Serikali iimaishe udhibiti wa mafuta na bidhaa zinazoingia nchini kwa matumizi ya ndani, na zinazopita kwenda nchi nyingine ili kuhakikisha kuwa zinalipiwa kodi stahiki.


(iii) Serikali iimarishe udhibiti wa ndani katika kuhakiki mikopo iliyopokelewa na taasisi nufaika kabla ya kuingiza kumbukumbu za madeni kwenye mfumo ili kuondoa mapungufu katika usahihi wa taarifa.


(iv) Kupitia Maofisa Masuuli, Serikali iimarishe udhibiti na utaratibu wa kufanya mapitio ya uandaaji wa mafao ili kuhakikisha kuwa kanuni na vigezo vya ukokotoaji na sheria vinazingatiwa ili kuepuka ucheleweshaji wa mafao ya hitimisho la kazi na hasara kwa Serikali.


(v) Serikali itoe kwa wakati fedha za utekelezaji wa miradi ya barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania kama ilivyoidhinishwa na bunge ili kuepuka malipo ya ziada yanayotokana na riba.


(vi) Kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa, Serikali ihamishe mali na madeni yote yanayohusiana na miradi ya barabara kwenda Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini; na Ofisi ya Rais - TAMISEMI inapaswa kufuatilia utekelezaji huo.


(vii) Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa iharakishe zoezi la usajili na utengenezaji wa vitambulisho vya Taifa. Pia, itathmini utendaji kazi wa mkandarasi ili kuweza kuamua iwapo imuongezee muda wa mkataba au iingie makubaliano na mkandarasi mwingine. 


(viii)Serikali kupitia Taasisi zake iepuke kufanya manunuzi toka chanzo kimoja au kushindanisha vyanzo vichache endapo bidhaa au huduma zinazotakiwa haziendani na zile zilizotajwa katika Kanuni ya 159 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma za Mwaka 2013. Hii itasaidia kuwa na usawa na uwazi katika manunuzi ya Umma. Pia, ihakikishe kuwa manunuzi yote yanapata vibali vya Bodi za Zabuni kabla ya kufanyika kwa manunuzi ili kuhakikisha uwepo wa thamani ya fedha katika manunuzi.

(ix) Serikali ihakikishe malipo yote yanafanyika kwa mujibu wa mikataba iliyosainiwa baina ya Taasisi za Serikali na watoa huduma. Vilevile, Taasisi za Serikali zihakikishe zinadai na kupatiwa stakabadhi za kielektroniki pindi zinapowalipa wazabuni ili kuzuia ukwepaji wa kodi.


(x) Uongozi wa Vyama vya Siasa uhakikishe kuwa udhibiti unaanzishwa na kuimarishwa, hasa kwenye malipo, ili malipo yote yawe na vielelezo na nyaraka toshelezi, zikiwamo risiti za kielektroniki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com