Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Ripoti ya CAG: MATOKEO YA KAGUZI MAALUMU ( MFUMO USIOFANYA KAZI SHIRIKA LA BIMA LA TAIFA; MALIPO HEWA YALIYOFANYWA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA)

8.1 Utangulizi
Sura hii inawasilisha matokeo ya ukaguzi maalumu uliofanywa na Ofisi yangu. Ukaguzi ulifanyika kuhusiana na Ununuzi wa Mfumo usiofanya kazi katika Shirika la Bima la Taifa; Malipo Hewa kwa Mzabuni yaliyofanywa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya;



Udanganyifu katika Malipo ya shilingi milioni 267.89 kwenye Akaunti ya Matumizi Mengine katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo; na Malipo Hewa katika Kandarasi za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’. Maeneo mengine ambayo Ukaguzi Maalumu ulifanyika ni Ununuzi wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS) katika Jeshi la Polisi Tanzania; ujenzi wa Uwanja wa Ndege Songwe; na Ununuzi wa Sare za Askari Polisi uliofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania.

Ndugu Waandishi wa Habari, 
Ofisi yangu ilifanikiwa kufanya kaguzi maalumu katika Taasisi mbalimbali za Umma. Yafuatayo ni baadhi ya mapungufu niliyoyabaini. 

8.2 Shirika la Bima la Taifa kuwa na Mfumo usiofanya kazi ulionunuliwa kwa Gharama ya Dola za Marekani Milioni 3.59  

Shirika la Bima la Taifa liliingia mkataba wa kununua mfumo wa ‘Genisys’ tarehe 18 Juni, 2012 kwa ajili ya kufungamanisha kazi kuu tatu za Shirika ambazo ni Bima ya Maisha, Bima zisizo za Maisha, na Uhasibu. Shirika liliukubali na kuupokea mfumo na kulipa Dola za Marekani milioni 3.59. Hata hivyo, ukaguzi wangu umebaini kuwa mfumo huo haufanyi kazi kikamilifu, hivyo kusababisha Shirika kutumia mfumo mwingine uitwao UNISYS. Kutokana na changamoto hizi, thamani ya fedha zilizotumika katika kununua mfumo huu haijaweza kupatikana kwani malengo ya kununuliwa kwake hayakufikiwa.   

8.3 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kufanya Malipo Hewa ya Shilingi Bilioni 2.61 kwa Mzabuni 

Katika uchunguzi wa vitabu vya fedha, taarifa za benki, na hati za malipo za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nilibaini kuwepo kwa malipo ya kiasi cha shilingi bilioni 3, kati ya malipo hayo shilingi bilioni 2.61 yalikuwa malipo hewa; shilingi milioni 350.87 ni malipo ambayo walipwaji walishindwa kubainika; na shilingi milioni 42.6 hazikuweza kuthibitika kupokelewa na walipwaji. Malipo haya yalitakiwa kulipwa watoa huduma za afya kwa kutumia hundi zilizofungwa lakini yalifanywa kwa fedha taslimu kinyume na Kanuni za Fedha za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

8.4 Udanganyifu katika Malipo ya Shilingi Milioni 267.89 kwenye Akaunti ya Matumizi Mengine katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo

Ndugu Waandishi wa Habari,
Nilikagua malipo mbalimbali katika Akaunti ya Matumizi Mengine na nilibaini kuwa kwa nyakati tofauti kuna watumishi walianzisha, kupitisha, na kufanya malipo ya ya shilingi milioni 267.89 ambayo hayakuwa na viambatisho husika na mengine yalikuwa na viambatisho vyenye shaka. 

8.5 Upotevu wa Mapato ya Zaidi ya Shilingi Bilioni 3.4 katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’

Mapitio ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani yalibaini mapungufu mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kushindwa kuwasilisha vitabu 425 vya kukusanyia mapato. Mambo mengine yaliyobainika ni pamoja na:
(a) Upotevu wa mapato ya ndani ya Halmashauri ya jumla ya shilingi bilioni 1.04 yaliyokuwa yanakusanywa na mawakala; na 

(b) Kutopatikana kwa nyaraka muhimu za makampuni ya mawakala wa ukusanyaji wa mapato kwa mikataba yenye thamani ya shilingi bilioni 2.36

8.6 Malipo Hewa ya Shilingi Milioni 73.45 katika Kandarasi za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’

Ukaguzi maalumu umebaini kuwa fedha kiasi cha shilingi milioni 73.45 za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji zililipwa kwa wakandarasi kama dharura bila kuwepo kazi za dharura. Ukaguzi umebaini kutokuwepo kwa ushahidi wowote wa kufanyika kwa kazi hiyo, na hivyo kudhihirika kuwa matumizi hayo ni hewa. 

8.7 Ununuzi wa Mashine za Mfumo wa Kidigitali wa Usajili wa Wapiga kura (BVR) Uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi 

Nilibaini kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilinunua mashine za BVR 8,000 kwa ajili ya usajili wa wapiga kura, ambapo kati ya hizo, mashine 5,000 hazikukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba hivyo kusababisha kutolandana kimatumizi na vile vilivyonunuliwa hapo awali na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Wakala wa Taifa wa Usajili, Ufilisi, na Udhamini (RITA). Kutolandana huku kumeisababishia Serikali hasara ya shilingi milioni 862.08 zilizotumiwa na NIDA kununulia leseni mpya za “Windows” na “Biometric Algorithms” ili kubadilisha mashine 5,000 zilizopokelewa kutoka NEC ziweze kufanya kazi na mfumo wa BVR wa NIDA.

Aidha, nilibaini kuwa mzabuni alilipwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 72.30 badala ya Dola milioni 72.15, kiasi ambacho kilikuwa bei ya mkataba hivyo kuwa na ongezeko la Dola za Marekani 148,243.73. Pia, mafunzo kwa maofisa 15 wa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi hayakufanyika licha ya mzabuni kulipwa Dola za Marekani 358,650 kwa ajili ya mafunzo hayo.

8.8 Ununuzi wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS) Uliofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Ukaguzi maalumu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole (AFIS) ulibaini mambo yafuatayo: 
(a) Mahitaji ya kitaalamu kutoka idara inayotumia mfumo huo hayakuzingatiwa wakati wa kutathmini na kutoa zabuni. 

(b) Malipo ya shilingi bilioni 3.30 yalifanyika kwa mzabuni kwa ajili ya huduma ya matengenezo na msaada wa kitaalamu wa Mfumo wa Utambuzi wa Alama za Vidole kwenye mikoa nane ya Kipolisi ya Temeke, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Kigoma, Geita, na Kinondoni lakini Jeshi la Polisi lilishindwa kuthibitisha kuwa matengenezo hayo na msaada wa kitaalamu ulifanyika. 

(c) Vifaa vya Utambuzi wa Alama za Vidole vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.73 havikufungwa kwenye magereza 35 yaliyoainishwa. Badala yake vilihifadhiwa katika Ofisi ya Upelelezi, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. 

(d) Malipo ya shilingi milioni 604.39 kwa ajili ya mafunzo kwa wataalamu 30 hayakufanyika. 

(e) Jeshi la Polisi lilishindwa kuionesha timu yangu ya ukaguzi zilizo monita 58 za kompyuta aina ya Dell zenye thamani ya shilingi milioni 159.16 zilizopelekwa kwenye Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi (Forensic Unit). Pia, monita 213 za kompyuta aina ya Dell zililipiwa kiasi cha shilingi milioni 195.22 kwa mzabuni Lugumi Enterprises Limited lakini mzabuni hakuzileta. 

8.9 Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Songwe

Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika ukaguzi maalumu wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Songwe, Mbeya nilibaini mambo yafuatayo: 
(a) Malipo ya jumla ya shilingi bilioni 1.43 yalifanyika mara mbili kwa udanganyifu kupitia maofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA). Aidha, jumla ya shilingi bilioni 1.95 zililipwa bila ya kuwepo kwa jedwali la vipimo na hati za madai zilizoidhinishwa na mhandisi mshauri. 

(b) Kati ya malipo ya awali ya shilingi bilioni 1.70 alizolipwa mkandarasi kwa ajili ya kuanza shughuli za ujenzi, ni shilingi milioni 176.56 tu ndizo zilizorejeshwa. Hivyo, bakaa ya shilingi bilioni 1.52 haikurejeshwa hadi ukaguzi huu unafanyika. 

(c) Shilingi milioni 570.50 zililipwa zaidi ya gharama zilizoidhinishwa na mhandisi mshauri. 

(d) Jumla ya shilingi bilioni 5.48 zililipwa kwa mkandarasi bila ya kuidhinishwa na mhandisi mshauri. 

8.10 Ununuzi wa Sare za Askari Polisi Uliofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania

Katika ukaguzi huu maalumu, nilibaini kuwa Jeshi la Polisi Tanzania lililipa jumla ya shilingi bilioni 16.66 bila ya kuwapo na ushahidi wa uagizaji na upokeaji wa Sare za Askari Polisi kwa Boharia Mkuu wa Jeshi la Polisi. 

Pia, nilibaini maoni ya Kisheria ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanayohusu uwasilishaji wa Kiapo cha Nguvu ya Kisheria (Power of Attorney) na leseni halali ya biashara hayakuzingatiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani wakati wa kusaini Mkataba Na. ME.014/PF/2015/2016/G/30 Lot 2 uliohusu ununuzi wa sare za askari polisi. 

8.11 Mapendekezo 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kutokana na matokeo ya ukaguzi maalumu nilioufanya katika maeneo yaliyoelezwa, ninaishauri Serikali:
(i) Kuchukua hatua stahiki za kisheria na kinidhamu dhidi ya maofisa waliohusika katika ubadhilifu wa Mali za Umma.  Pia, Mamlaka husika zihakikishe kuwa mianya yote niliyobainisha wakati wa ukaguzi inayopelekea upotevu wa Mali za Umma inazibwa.

(ii) Kupitia Shirika la Bima la Taifa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, iwasiliane na wazabuni ili kuhakikisha kwamba masuala yote yaliyobaki kama ilivyooneshwa katika Hati za Mahitaji ya Kazi za Mifumo yanatatuliwa na kwamba mifumo hiyo inafanya kazi kikamilifu kama ilivyotarajiwa.

(iii) Kupitia Jeshi la Polisi Tanzania, ihakikishe kuwa vifaa vya Utambuzi wa Alama za Vidole vinafungwa katika maeneo husika na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com