Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilayani Kibondo mkoani Kigoma wametakiwa kuacha kupokea rushwa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuja kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na serikali kuu.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma Louis Bura wakati wa ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya tawi hadi kata na jumuiya zake na kuwajengea weredi na uelewa wa namna gani ya kuongoza ambapo aliwataka kuwaacha wananchi kuchagua kiongozi aliye bora na sio kumpendekeza kiongozi ambaye amepita na kuwagawia rushwa katika kata zao.
Alisema kuelekea uchaguzi mwaka huu na mwaka 2020 ni lazima viongozi wa chama wawe makini na viongozi wanaotaka kugombea kwa kuwa watapita mitaani kuwashawishi kwa kuwa wao ndio wapiga kura wa kwanza na kuwataka viongozi hao kuacha kuchochea kiongozi flani apitishwe kwa kuwa katoa pesa.
Bura alisema kiongozi mtoa rushwa hafai katika uchaguzi huu kwa kuwa anakuwa ana lengo la kujitengenezea masilahi yake binafsi.
"Tunafahamu wapo baadhi ya watu wanaotaka kugombea wanapita wanawashawishi muwachague, niseme tu kwa yeyote tutakaemkamata hatutasita kumuadhibu na ikiwezekana tutashirikiana na viongozi wa chama kumfuta kabisa katika watu wanaogombea, hatutaki viongozi wanaotoa rushwa, kiongozi apite kwa kujiamini mwenyewe na kuaminiwa na wananchi", alisema Bura.
Akiwakaribisha watoa mada walioandaliwa katibu wa CCM Wilaya ya Kibondo Stanley Mkandawile aliwataka viongozi wa matawi na kata kuwa wa kweli kutoa tathmini za kweli ni mgombea gani anakubalika na Wananchi ilikuhakikisha wanakipatia ushindi wa kutosha chama.
Alisema viongozi wanaotoa fedha kuwashawishi wapiga kura kuwachagua hawafai na viongozi ambao hawakubaliki kwa wananchi hawafai, lazima viongozi wa chama wa kata na matawi, kupita kwa wananchi kujua ni kata gani chama kina mgombea ambaye anakubalika na kata gani ambako kuna changamoto kiongozi aliyepo hakubaliki.
Aidha Mkandawile alisema lengo la chama ni kuhakikisha kata 19 na vijiji vyote vya kata hizo wanapata ushindi pamoja ili kufanikisha hilo ni lazima viongozi kupata idadi ya wanachama waliopo katika kata zao na kutatua kero zote ambazo zinaweza kusababusha chama kukosa ushindi.
Katibu kata ya Misezero,Benjamini Mlinjie alisema semina ya kuwajengea uwezo imewafungua fikra za uongozi na mpaka sasa wamejipanga kushirikiana na TAKUKURU kuwafichua wale wote wasiojiamini na wanataka kutoa rushwa ili wapitishwe.
Alisema wapo baadhi wanatabia hizo na kwa sasa watahakikisha viongozi wote wanaopita wana uwezo wa kuongoza na wanapita kutokana na wananchi wanavyowakubali na sio kwa sababu ya kutoa rushwa.
Alisema wako tayari kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa,Dkt. John Pombe Magufuli kuhakikisha chama kinapata viongozi waadilifu na wanaokubalika na wananchi kwa kuwa chama kina hazina ya kutosha.
Na Rhoda Ezekiel Kigoma - Malunde1 blog
Social Plugin