Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI IMEANZA MAZUNGUMZO NA NCHI ZA MISRI NA ALGERIA KUANDAA MAKUBALIANO YA KUUZA TUMBAKU YA TANZANIA

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeanzisha mazungumzo na nchi wanachama wa COMESA na nchi kama Misri na Algeria kupitia balozi zake ili kuandaa Makubaliano Maalum (Bilateral Agreement) yatakayoiwezesha Tanzania kupeleka tumbaku kwa kodi nafuu.

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) ameyasema hayo bungeni Jijini Dodoma leo tarehe 17 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mhe Edwin Amandus Ngonyani Mbunge wa Namtumbo aliyetaka kufahamu Wizara ya Kilimo inashirikianaje na Wizara nyingine zinazohusika na uwekezaji wa mambo ya nje kutafuta soko la tumbaku nchini Misri badala ya kulazimika kutumia nchi za Uganda na Kenya pekee.

Mazungumzo hayo yamefikia hatua nzuri na matarajio ni kufungua milango ya soko hilo na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima na taifa kwa ujumla. Aidha, Makubaliano hayo yakikamilika Tanzania inaweza pia kuuza chai nchini Misri na Algeria kwa faida kuliko ilivyo hivi sasa au badala ya kuuza chai kupitia mnada wa Mombasa nchini Kenya.

Mhe Bashungwa alisema kuwa mwaka 2014/2015 uzalishaji wa tumbaku ya moshi (Dark Fire Cured Tobacco – DFC) ulisimama mkoani Ruvuma kutokana na kukosa soko.

Hata hivyo, Jitihada za Serikali ikawezesha Kampuni ya Premium Active Tanzania Limited (PATL) kuonesha nia ya kununua tumbaku hiyo ya DFC ambayo nchini Tanzania huzalishwa katika Wilaya ya Namtumbo na Songea Vijijini Mkoani Ruvuma.

Alisema Kampuni hiyo ilieleza kuwa lipo soko kubwa la tumbaku aina ya DFC nchini Misri na Algeria lakini tumbaku ya Tanzania inauzwa kwa bei ya juu kutokana na kodi inayotozwa ikilinganishwa na aina hiyo ya tumbaku kutoka nchi za Uganda na Kenya kwa kuwa nchi hizo (Uganda, Kenya, Algeria na Misri) ni wanachama wa jumuiya ya COMESA na kwa hiyo kodi za kuingiza tumbaku, chai na bidhaa nchini Algeria na Misri kutoka Uganda na Kenya ni za chini.

Mhe Bashungwa alisisitiza kuwa, ili Tanzania iuze tumbaku, chai na bidhaa nyingine katika nchi za Algeria na Misri kwa faida, inatumia nchi zilizo kwenye jumuiya hiyo kama Uganda na Kenya.

Kadhalika, Mhe Bashungwa alisema kuwa Wizara ya Kilimo inaendelea kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo tayari soko la mahindi limepatiwa ufumbuzi kwa Wizara kuingia mkataba wa mauziano na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuingia mikataba ya masoko ya uhakika kwenye mazao ya kimkakati na mazao mchanganyiko.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com