Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUAJIRI WATUMISHI WAPYA 44,807 KATIKA MWAKA WA FEDHA 2019/20

Bunge limeelezwa kuwa katika mwaka wa fedha 2019/20, serikali itaajiri watumishi wapya 44,807 wa kada mbalimbali.

Miongoni mwa kada zitakazoajiri watumishi wengi ni Elimu (13,526), Afya (9,467), Jeshi la Polisi (3,725).

Kada zingine ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi (2,141), Magereza (685), Jeshi la Zimamoto na Uhamiaji (500), Hospitali za mashirika ya dini na hiari (1,262) na pia watumishi 13,002 wa kada nyingine wakiwamo wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/2020.

Alisema mbali na kuajiri, pia watumishi 290,625 watapandishwa vyeo kulingana na maelekezo yatakayotolewa.

Aidha, alisema bodi itafanya utafiti wa hali ya mishahara na masilahi katika vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni Polisi, Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kushauri namna bora ya kutoa motisha.

“Utoaji motisha utazingatia viwango stahiki vya kuongeza ufanisi katika kazi za vyombo hivyo,” alisema.

Mkuchika alisema Bodi ya Mshahara na Masilahi katika Utumishi wa Umma inatarajia kuandaa taarifa nne za gharama ya maisha ambazo zitatumika kushauri kiwango cha mshahara unaoendana na gharama za maisha kwa watumishi wa umma.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com