Na Shamim Nyaki – WHUSM,Dodoma.
Serikali imejipanga kuanzisha Makumbusho Maalum katika Uwanja wa Taifa ya kuhifadhi taarifa na picha za wanamichezo walioliletea Taifa heshima katika mashindano mbalimbali ya Kimataifa.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza alipokuwa akijibu swali la msingi la Mhe.Ester Mahawe (Viti Maalum) kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyeuliza ni lini serikali itaandaa utaratibu wa kuwaenzi wanariadha nchini.
Mhe.Shonza alieleza kuwa Serikali inawatambua na kuwaenzi wanamichezo wote ambao wameletea nchi sifa kubwa wakiwemo Mwanariadha Filbert Bayi aliyevunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1500 mwaka 1974 ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Jumaa Ikanga mshindi wa Medali ya Shaba Mashindano ya All- Africa Games mwaka 1978 na Medali ya Fedha Michezo ya Olimpiki 1980 kwa mbio za mita 5000 hivi sasa ni Kocha wa Riadha wa Taifa Brunei.
“Kanuni ya mafanikio katika michezo popote duniani yanatokana na mwanamichezo mwenyewe kuonyesha juhudi binafsi za kujituma na kujipambanua kuwa bora miongoni mwa wanamichezo wengine,hivyo wanamichezo lazima waendelee na jitihada za kujituma.”alisema Mhe.Shonza.
Aidha, Mhe.Shonza alipojibu swali la nyongeza la Mhe.Anna Gidarya Mbunge Viti Maalum (CHADEMA) Mkoa wa Manyara aliyeuliza ni lini Serikali itaboresha miundombinu ya viwanja katika vyuo vya elimu ya juu, ameeleza kuwa suala la kuboresha miundombinu linahitaji ushirikiano kati ya Serikali na wadau hivyo amewataka waheshimiwa wabunge kuona changamoto hiyo na kuifanyia kazi.
Social Plugin