Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendelo ya Jamii, imeishauri Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya elimu ya Juu (HESLB) kuweka fedha za kujikimu za wanafunzi moja kwa moja kwenye akaunti zao binafsi ili kuepuka changamoto zinazojitokeza.
Akisoma hotuba ya Kamati hiyo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, bungeni leo Aprili 29, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Nkamia amesema wanafunzi wamekuwa wakichelewa kupata fedha za kujikimu kutokana na changamoto mbalimbali zinazokabili vyuo vyao na baadhi ya benki nchini.
Amesema kutokana na baadhi ya vyuo kuwa na madeni ya mikopo benki, fedha za kujikimu za wanafunzi zimekuwa zikizuiwa na hivyo kusababisha hali ngumu kwa wanafunzi.
Nkamia ambaye pia ni Mbunge wa Chemba,(CCM) amesema Kamati imeshauri serikali kuhakikisha inaboresha maslahi ya wahadhili na watumishi wa vyuo vikuu, hususani posho ya nyumba ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Social Plugin