SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO WANANCHI KATIKA MASUALA YA MAFUTA, GESI


Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali  kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea na mkakati wake wa kuwajengea uwezo wananchi  illi waweze kupata taaluma na kuweza kushiriki kwenye sekta ya mafuta na gesi.

Akizungumza  Bungeni leo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Nishati,  Subira Mgallu alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kuvitumia vyuo vilivyopo nchini kuwajengea uwezo wa kitaaluma wananchi katika masuala ya utafutaji,  uendelezaji,  uchakataji,  usafirishaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia.

Naibu Waziri Mgallu alisema, “Kwa mfano mwaka 2010 Kampuni ya Petrobras ilitumia dola za kimarekani 350,000 sawa na shilingi milioni 780 kufundisha na kukipatia Chuo cha VETA Mtwara vifaa vya mafunzo. Aidha, kupitia mpango huo, wanafunzi 50 na wakufunzi 2 walifundishwa kwenye fani ya umeme na makanika”.

Aidha, Kampuni ya Statoil imekuwa ikifadhili mafunzo mbalimbali kwa ngazi ya vyuo, ambapo mwaka 2013 ilifadhili wananchi 9 kusoma Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika masuala ya fedha  na uchumi wa mafuta ya gesi asilia.

Sambamba na hilo, mwaka 2012  Kampuni ya BG  iliendesha mafunzo mbalimbali katika Chuo cha VETA mkoani Mtwara, ikiwa ni pamoja na ufadhili wa mwaka 2012/2013 uliotolewa na iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini  kwa wanafunzi 50 katika chuo hicho.

Naibu Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) imefungua klabu 32 za mafuta na gesi katika shule za Sekondari za mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kutoa elimu inayohusu tasnia ya mafuta na gesi asilia pamoja na namna inavyoweza kuwanufaisha kupitia fursa zinazotengenezwa na tasnia hiyo katika maeneo yao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post