Na Lusungu Helela, Dodoma
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameagiza minada yote ya mifugo iliyokamatwa hifadhini, baada ya serikali kushinda kesi mahakamani ifanyike nje ya hifadhi ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa wahifadhi hukamata mifugo hiyo ili waweze kujiuzia wenyewe.
Pia, ameagiza minada hiyo itangazwe katika vijiji kabla ya tarehe ya kufanyika kwa lengo la kuwajulisha Wananchi hata kwa wale walioshindwa kesi hizo, ili waweze kushiriki katika minada hiyo huku Mkuu wa Wilaya husika ashirikishwe ipasavyo kwenye minada.
Akizungumza na viongozi wa vijiji 15 katika Kijiji cha Kisondoko, ambavyo ni miongoni mwa vijiji vilivyokutwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero lililopo katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, Kanyasu alisema minada hiyo isifanyike kwa usiri badala yake iwe wazi nje ya hifadhi ili kutoa fursa kwa yeyote kushiriki.
Akizungumzia kuhusu ugumu wa kupata vibali vya kuingilia hifadhini wakati minada ilipokuwa ikifanyikia ndani, Kanyasu alisema kabla ya agizo hilo wananchi waliokuwa wakishiriki katika minada hiyo, walihitajika wawe na vibali vya kuingilia hifadhini la sivyo walikuwa wakikatwa kwa kosa la kuingia hifadhini bila kibali.
Alisema, endapo minada hiyo itafanyika kwa uwazi na nje ya
hifadhi kutasaidia kuepusha shutuma nyingi, zikiwemo za rushwa zinazowakabili wahifadhi kuwa wamekuwa wakishiriki kuwatafuta wanunuzi wa ng'ombe kutoka mikoa ya mbali kwa makubaliano ya kulipwa mara baada ya mnada.
Naibu Waziri huyo alisema, kitendo cha minada hiyo kuanza kufanyika nje ya hifadhi kutasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi, ambao wamekuwa wakidai pindi mifugo yao inapotaifishwa wamekuwa hata hawajulishwi, lakini wafanyabiashara wakubwa ndiyo wamekuwa na taarifa.
Alisema, wananchi ambao mifugo yao imekuwa ikikamatwa na baadaye kutaifishwa wamekuwa na chuki na wahifadhi huku wakiwatuhumu kuwa wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara hao kwa kuwajulisha, ili wafike hifadhini kwa ajili ya kuinunua.
Katika hatua nyingine, Kanyasu amewaonya askari wa wanyamapori wenye tabia ya kuvizia ng'ombe wakiwa mpakani kati ya kijiji na hifadhi na kisha kuwasukumia ng'ombe hao ndani ya hifadhi ili wazikamate kuwa vitendo hivyo, havikubaliki na si kazi waliyotumwa na serikali.
Social Plugin