Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali inayo dhamira ya kukamilisha skimu zote za umwagiliaji ambazo utekelezaji wake haujakamilika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma jana tarehe 15 Aprili 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe Azza Hillal Hamad aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katika Kijiji cha Ishololo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Mhe Mgumba amesema kuwa Skimu hiyo ipo miongoni mwa skimu za umwagiliaji zitakazopewa kipaumbele katika kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji (Irrigation Master Plan 2018 - 2025) ambao kwa sasa umeanza kutekelezwa.
Alisema kwa kuzingatia umuhimu wa miradi hiyo ukiwemo mradi wa umwagiliaji Ishololo, tayari Serikali imekwishaanza mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la JICA kwa lengo la kuboresha miradi yote ambayo haijakamilika na ile inayofanya kazi chini ya ufanisi uliokusudiwa.
Naibu Waziri huyo wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) alisema kuwa mradi wa ujenzi wa bwawa wa Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni moja kati ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo katika Wilaya (DASIP) chini ya iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Alisema Utekelezaji wa Mradi huo ulifikia ukomo wake mwezi Desemba 2013 ambapo Benki Maendeleo ya Afrika ilisitisha kutoa fedha za utekelezaji wa miradi wakati utekelezaji wake ukiwa haujakamilika.
Social Plugin