Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFUNGUKA KUHUSU ELIMU YA MSINGI KUISHIA DARASA LA SITA


Serikali imesema kwa sasa hakuna haja ya kubadilisha muda wa kuhitimu elimu ya msingi kwa sababu imebaini muda wa miaka saba unaotumika si kitu kibaya.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha leo Aprili 17 wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi ambalo limehoji, serikali inazunhgumziaje kuhusu kutotekelezwa kwa sera ya elimu ya kuishia darasa la sita badala ya darasa la saba.

Akijibu swali hilo, Ole Nasha amesema sera siyo msahafu na serikali inaweza kuibadilisha wakati wowote kadri itakavyoona inafaa kwa wakati husika, “Kwa wakati huu tumeona elimu kuanzia darasa la kwanza hadi la saba siyo kitu kibaya. Hatuna haja ya kubadili ndiyo maana tumebakia na mfumo wa zamani”, amesema Ole Nasha.


Amesema kwa hatua hiyo Serikali haijavunja sheria na kwa sasa ipo katika mapitio kwa mambo mapya yaliyoko katika sera ya elimu ambayo wanaona hawataweza kutekeleza.

Amesema Serikali inazingatia ubora wa elimu ndiyo maana kumetokea mabadiliko makubwa katika idara ya udhibiti wa elimu.



Ameongeza kuwa, wameanza utaratibu mpya wa udhibiti ubora wa elimu kwa ushirikishwaji ambao unawaleta wadau wote kwa pamoja, pia wanahakikisha waratibu wa elimu wanapata vifaa na ofisi ili kusimamia vizuri kuhakikisha elimu inakuwa bora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com