Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Ni tukio la kihistoria ambapo leo, Aprili 24, 2019, Serikali ya Tanzania, imetoa dola za Marekani milioni 309.65, sawa na takriban shilingi bilioni 688.65, fedha zake za ndani, kama malipo ya awali kwa Mkandarasi - Arab Contractors ya Misri, wanaojenga mradi wa kuzalisha umeme unaotokana na maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, mkoani Pwani.
"Haijapata kutokea katika historia ya nchi hii Serikali kutoa fedha nyingi za malipo ya awali ya kiasi kama hiki cha shilingi bilioni 688.65 katika mradi wa aina yoyote uliowahi kutekelezwa hapa nchini isipokuwa huu" alisema Bw. Doto James, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.
Bw, Doto James, ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, alimkabidhi hundi kifani ya dola za Marekani milioni 309.65, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, ambaye alimkabidhi hundi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO, Dkt. Alexender Kyaruzi, ambaye pia alimkabidhi hundi hiyo Naibu Mkurugenzi wa Ujenzi wa mradi huo Mhandisi Mohamed Hassan, kwa niaba ya kampuni za Arab Contractors (Osman A. Osman & Co na Elsewedy Electric S.A.E (AC-EE JV).
Alisema kuwa kiasi kilichotolewa cha shilingi bilioni 688.65 ni sawa na asilimia 70 ya zaidi ya shilingi trilioni 1 ya malipo ya awali yanayotakiwa kutolewa ya asilimia 15 ya mradi huo ambao hadi kukamilika kwake ndani ya miaka mitatu ijayo, unakadiriwa utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 6.6.
Bw. James amezitaja baadhi ya faida za mradi huo utakapo kamilika na kuzalisha megawati 2,115 za umeme kuwa ni pamoja na nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika, kuongezeka kwa uwekezaji katika sekta ya viwanda vitakavyo chochea uzalishaji wa bidhaa, ajira pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo yanayozunguka mradi na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
"Ninamtaka Mkandarasi akamilishe mradi huu kwa wakati na kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba ili mradi utakapo kamilika uwe kichocheo muhimu cha kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025" alisisitiza Bw. Doto James
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu Na. 14.2 cha Mkataba, malipo ya awali ya Mkandarasi ni asilimia 15 ambazo zimegawanywa katika sehemu mbili ambapo asilimia 70 zinalipwa kwa kutumia sarafu ya kigeni (dola za Marekani 309.645m) na asilimia 30 zitalipwa kwa fedha za ndani ambazo zitalipwa baada ya Mkandarasi kukamilisha taratibu za kimkataba zinazohusu malipo hayo.
"Ninao uhakika kwamba malipo haya ya awali yatamwezesha Mkandarasi kukamilisha taratibu za kupeleka vifaa katika eneo la mradi na kuanza ujenzi mara moja kwa mujibu wa Mkataba.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Alexender Kyaruzi, alisema uzalishaji wa umeme hapa nchini umefikia megawati 1600 na kwamba kuongezeka kwa megawati nyingine 2,115 ni hatua kubwa na ya furaha na amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutekeleza mradi huo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi Mohamed Hassan ameishukuru Serikali na wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata na amewahakikishia watanzania kwamba mradi huo utatekelezwa kwa haraka na kwa viwango ili kutimiza matarajio ya nchi ambayo ni maendeleo.
Social Plugin