Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHAHIDI: NYAMA NA NYWELE SEHEMU ZA SIRI ZILITHIBITISHA UHUSIANO WA MWANAFUNZI HUMPHREY MAKUNDI NA WAZAZI WAKE

Na Dixon Busagaga
Mkemia kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ,Hadija Mwema ameieleza mahakama kuu kanda ya Moshi  kuwa Vinasaba (DNA) vya sampuli zilizochukuliwa katika mwili wa anayetajwa kama Humphrey Makundi vimeshabihiana na Vinasaba (DNA)  vya Joyce na Jackson Makundi ambao wanatajwa kama wazazi wa marehemu .


Dkt Mwema ambaye ni shahidi wa 12 katika shauri la mauji ya kukusudia ya Mwanafunzi Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Scholastica aliieleza makama kuwa sehemu iliyotoa majibu ya vipimo vya DNA ilikuwa ni Nyama na Nywele katika sehemu ya uume vilivyolinganishwa na Ute wa mate pamoja na Damu vya Joyce na Jackson Makundi.

Eneo la sehemu ya nyama na Nywele katika eneo la uume ni miongoni mwa sampuli zilizotumika kwa ajili ya vipimo kati ya sampuli 15 ambazo 10 kati ya hizo zilichukuliwa mwilini huku nyingine zikiwa ni viatu na nguo.

Baadhi ya sampuli nyingine zilizotajwa mahakamani hapo katika ripoti ya vipimo vya DNA,ni pamoja na Ngozi ya Kisigino,Mfupa wa Paja,Mfupa wa Kifua ,kipande cha nyama ya tako,viatua jozi mbili ,maji mazito yanayopatikana katikati ya mfupa vyote hivi vikiwa ni vya marehemu.

Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu,Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,Dar Es Salaam ,Firmin Matogoro ,shahidi huyo aliiomba mahakama kuu kanda ya Moshi kupokea Ripoti ya Vipimo vya Vinasaba (DNA) iwe sehemu ya kielelezo katika ushahidi wake ambacho kilipokelewa na kupewa namba nne.

Akiongozwa na Wakili wa serikali Mwandamizi ,Abdalah Chavula ,Mwema alieza kuwa baada ya kufanya vipimo vya Sampuli mbalimbali matokeo yaliyoonesha zilichukuliwa katika mwili wa Binadamu.

Mapema Shahidi wa 11 katika shauri hilo linalovuta hisia za watu ,Jackson Daudi aliyejitamburisha kama mbebaji wa mizigo katika kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Moshi Ciment aliwasilisha Panga mahakamani hapo lipokelewe kama kielelezo katika ushahidi wake.

Akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Joseph Pande ,Daudi ambaye wakati huo alikuwa akifanya shughuli ya ulinzi katika shule ya sekondari ya Scholastica iliyopo Himo katika wilaya ya Moshi ambako alikuwa akisoma mwanafunzi Humphrey Makundi.

Alieleza kuwa Novemba 9 mwaka 2017 alifika katika shule hiyo akitokea Kahama ,mkoani Shinyanga ambako alifanya kazi ya ulinzi katika kampuni ya Solex Security Ltd kabla ya kukutana na mtu aliyemtaja kama mtoto wa Edward Shayo ambaye alimuunganisha kwenda kufanya kazi katika shule hiyo.

Daudi aliileza Mahakama sababu za kuacha kazi katika kampuni yake hiyo ya awali ilikuwa ni kutofautiana na muajiri wake baada ya kushindwa kumlipa mshahara wa mwezi mmoja ndipo alipoamua kuchukua vitu katika kampuni yake na kuvipeleka kituo cha Polisi.

“Baada ya kuelewana na mwajiri wangu na kunipa pesa na kutoka kituoni ,nilikutana na mtoto wa Edward Shayo anaye ishi wilaya ya Kahama ,ni Traffic ,akaniambia atanipeleka kufanya kazi kwenye shule ya baba yake”alieleza Daudi.

Alieleza kuwa Novemba 10,2017  ikiwa ni siku ya pili tangu kufika shuleni hapo alikutana na  Edward Shayo  aliyewauliza kama walielewana bei ya kufanya kazi na majibu yake yalikuwa ni hapana.

“Alituuliza ,Mlitaka mlipwe shilingi ngapi ? tukamjibu  shilingi laki mbili “alieleza Daudi huku Wakili Pande akitaka kujua walikuwa wangapi ndipo akaeleza kuwa walikuwa wawili yeye na mwenzake aliyemtaja kwa jina moja na Thomas.

Alieleza kuwa Edward Shayo aneyatajwa kama mmiliki wa shule hiyo aliwawambia kuwa atawalipa shilingi laki moja na wao walimueleza kuwa awalipe kiasi cha sh laki moja na ishirini kiwango ambacho alikubaliana nacho na kutoa maelekezo ya kumuona mtu aliyeitwa Chacha.

“Chacha alikuwa n mlinzi ,baada ya kumuona tukaambiwa nendeni mkapumzike mida ya saa 12 twende tuakaonyeshwe eneo la kazi ,tulikabidhiwa nguo za kazi “alieleza Daudi.

Daudi ambye mkewe anafanya kazi ya usafi katika shule ya sekondari ya Scholastica alieleza kuwa utaratibu waliopewa haukuwa wa kulinda wezi na kwamba walilinda wanafunzi wa shule na kwamba hata wangeingia wezi wangepambana nao.

“Thomas rafiki yangu alibaki pale getini,mimi na Chacha tukaanza kuzunguka maeneo ya shule ,sikuwa na kitu chochote ,Chacha alikuwa akitumia Panga na Rungu “alieleza Shahidi huyo.

Alieleza kuwa Novemba 17,2017 baada ya kutoka eneo lao la kazi walienda kupumzika na Chacha  na baadae mtu aliyemtaja kwa jina la Mcha Mungu aliyekuwa mlinzi wa getini  alifika na kuwaita bila ya kuaeleza kuwa wanaitwa na nani.

“Tuliendelea kulala,Mchamungu akatuaita mara ya pili ,akaita tena Chacha Chacha mnaitwa ,tukaulizwa tunaitwa na nani? Akatuambia mnaitwa na maaskari ,tukaenda getini tukakuta askari wa kike “trafiki “ “alieleza Daudi .

Shahidi huyo alieleza kuwa baada ya kufika yule Askari aliuliza anaitwa nani ndipo alipomtajia majina yake ya Jackson Evarlist Daudi na kueleza kuwasio yeye huku akiluza Chacha ni nani.

“Alipouliza Chacha nikamnyooshea kidole huyo hapo,akauliza na Mchamungu? Nikamnyooshea kidole huyo hapo na siku hiyo ilikuwa ni zamu ya Mchamungu kukaa getini” alieleza Daudi.

Mnamo Novemba 18 ,2017 majira ya saa mbili za usiku ,Daudi alieleza kuwa ilifika gari aina ya Landcruser ikiwa na vioo vyeusi ndipo alipofungua mlango mdogo katika geti la kuingia shuleni hapo ndipo aliposikia sauti ikimueleza kuwa hawaingii ndani.

“Walikuwa ni maaskari wakafungua mlango wa gari, wakamtoa Chacha,Chacha akawaongoza maaskari mpaka pale Panga lilipokuwa ,Panga lilikuwa kwenye kabati ndani ya Chumba cha Mlinzi ,kilichopo geti kuu lakuingia shuleni”alieleza Daudi.

“Walivyokuta Panga askari wakaniuliza tangu nifike hapo sijawahi kulishika hilo Panga au kulikamata nikasema hapana,nikaulizwa Panga la nani? Chacha mwenyewe kwa kinywa chake akakili Panga la kwangu”aliongeza Daudi.

Alieleza kuwa kuna Rungu lilikuwa juu ya meza ambapo pia askari walitaka kujua endapo nimewahi kulishika na majibu yalikuw ani hapana na kwamba baada ya hapo walipiga picha Panga na Rungu kisha wakaongozana na Chacha wakiwa na vitu hivyo.

Daudi alieleza muonekano wa Panga ulikuwa wa rangi nyeusi huku likiwa imemeguka kidogo huku akiionesha mahakama Panga hilo na baadae kuiomba mahakama itoe adhabu kutokana na Panga hilo.

Baada ya kutoa maelezo hayo Wakili Mkuu wa Serikali ,Pande aliwasilisha ombi mbele ya mahakama kupokea Panga hilo liwe sehemu ya kielelezo katika ushaidi wa Daudi jambo ambalo lilizua mabishano ya kisheria kwa pande zote mbili.

Wakili wa kujitegemea ,Gwakisa Sambo akiwasilisha ombi kwa Jaji,Mfawidhi,Matogoro alieleza kupinga ombi hilo akieleza sababu ya kuwa Wakili Pande si shahidi wa kutoa kielelezo hicho.

“Maombi yetu kwa upande wa prosecutor ,ni mahakama hii na mahakama zetu nchini ni shahidi pekee yake ambaye anaweza kuleta ombi hilo ,hivyo basi tunaomba ombi lake likataliwe.

Baadae alisimama wakili Pande na kuunga mkono hoja ya Wakili Sambo huku akileza kuwa ni kweli anayetoa kielelezo ni shahidi lakini anayeomba kielelezo kipokelewe ni upande wa Jamhuri na kwamba hivyo ni vitu viwili tofauti.

Shauri hilo linaendelea katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi,ambapo mashahidi wa upande wa jamhuri wameendelea kuwasilisha ushahidi wao.

Shauri la mauaji  ya mwanafunzi  Humphrey Makundi aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika  sekondari ya Scolastika imeanza kusikilizwa mfululuzo  likimkabili mmiliki wa shule hiyo ,Edward Shayo,Mwalimu wa nidhamu Labani  Nabiswa  na mlinzi wa shule ,Hamis Chacha.

 Upande wa Jamhuri katika Shauri hilo unawakilishwa na Wakili wa serikali Mkuu ,Joseph Pande,Wakili wa serikali Mwandamizi ,Abdala Chavula,Wakili wa serikali Mwandamizi ,Omary Kibwana  na Wakili wa serikali Lucy Kiusa.

Upande wa utetezi unawakilishwa na Wakili wa kujitegemea Elikunda Kipoko na Gwakisa Sambo wanaomtetea  mshtakiwa wa pili ,Wakili wa kijitegemea David Shilatu anayemtetea mshitakiwa wa kwanza na Patrick Paul anaye mtetea mshtakiwa wa tatu.

Mwisho.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com