Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewaondoa refa Abdallah Kambuzi na wasaidizi wake, Godfrey Msakila na Consolata Lazaro kwenye orodha ya marefa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara kwa mechi zilizobaki.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya watatu hao kuboronga katika maamuzi yao wakichezesha mechi ya Ligi Kuu baina ya KMC na Simba SC, zote za Dar es Salaam Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Simba SC iliendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu jana baada ya kuwachapa KMC 2-1, hivyo kufikisha pointi 66 baada ya kucheza mechi 26 na kupanda hadi nafasi ya pili ikiizidi kwa wastani wa mabao tu, Azam FC inayoangukia nafasi ya tatu, huku Yanga SC ikiendelea kuongoza kwa pointi zake 74 za mechi 32.
Lakini katika ushindi huo, ilionekana kabisa kulikuwa kuna mbeleko ya marefa, hatua ambayo imeifanya TFF isisubiri hadi Bodi ya Ligi itakapokuja kukaa baada ya muda mrefu na kuingilia kati kuwachukulia hatua waamuzi hao kwa kuutia doa mchezo.
Marefa hao wanadaiwa kuwapa Simba SC penalti mbili za utata jana ambayo moja walikosa, lakini pia kuwanyima KMC penalti na kutoa maamuzi mengine ya ovyo katika matukio ya kuotea.