Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) na shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na Mazingira (ENVICON) linaendesha semina ya siku tatu mkoani Shinyanga yenye lengo la kutoa elimu ya usalama sehemu za kazi kwa wafanyakazi wa kunyonya tope kinyesi na maji taka.
Semina hiyo inafanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) na kuwakutanisha pamoja wamiliki wa magari binafsi na serikali ya kunyonya kinyesi na wafanyakazi wao, watapishaji wa vyoo, pamoja na wadau mbalimbali kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, SHUWASA na EWURA.
Mkurugenzi wa ENVICON Profesa Karoli Njau amesema semina hiyo italenga zaidi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo utumiaji wa vifaa kinga wakati wa upakuaji wa kinyesi tope, usafirishaji na umwagaji salama kinyesi.
“Semina hii imelenga maeneo mbalimbali ikiwemo kuvaa vifaa vya usalama na kujikinga wakati wa kazi, na ikumbukwe kuwa haya ni matakwa ya sheria ya afya na usalama mahali pa kazi (OSHA 2003), Sheria ya afya ya jamii (PHA 2009) na sehria ndogo za Manispaa kwa wafanyakazi wote kuvaa vifaa kinga”, amesema.
Mmoja wa wamiliki wa magari ya kunyonya maji taka mkoani Shinyanga Ezekiel Gacha amewashukuru SNV pamoja na ENVICON kwa kuendesha semina hiyo ambayo ametaja eneo hilo kama lililosahaulika katika mnyonyoro wa kutunza mazingira na afya ya jamii mkoani Shinyanga.
“Unajua wadau wengi kwenye eneo hili la kunyonya kinyesi hawafuati kabisa taratibu zilizowekwa, wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea yaani hawatumii kabisa vifaa ambavyo wamepewa katika kufanya kazi hizi, sasa semina hii itawakumbusha na kuwafanya kuanza kutumia si kwa lengo la kutunza afya zao tu bali hata kwa wale ambao wanawazunguka,” Gacha amesema.
Awali akifungua semina hiyo Mshauri wa mradi kutoka SNV Elisekile Mbwile amesema hii ni sehemu ya mradi wa miaka mitano unaofanyika kwenye mikoa ya Shinyanga na Arusha na lengo lake mbali na kuwajengea uwezo, pia ni kuwabadilisha tabia ya kutotumia vifaa vya kujikinga wakati wa kupakua vyoo, makaro na kutupa tope kinyesi kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
“Hali ya utumiaji vifaa kinga wakati wa shughuli za upakuaji sio nzuri, katika watu kumi wanane hawatumii, ni matumaini yetu baada ya hii semina kutakuwa na mabadiliko makubwa kuanzia kwa wamiliki wa magari, waajiriwa na taasisi za serikali kwenye kusimamia jambo hilo”, amesema.
Semina hiyo iliyoanza Jumatano ya tarehe 10 mwezi huu inatarajiwa kumalizika Ijumaa ya tarehe 12 Mwezi huu.
Na Issack Msumba