Spika wa Bunge, Job Ndugai ameruhusu kuanza kusomwa kwa hotuba za Kambi rasmi za Upinzani Bungeni bila kuhaririwa kufuatia kambi hizo kugoma kusoma hotuba zao mara mbili mfululizo kwa kile kilichoelezwa waandaji kuwa wamekuwa wakitumia maneno ambayo yanaonekana kuwa na ukakasi.
Maamuzi hayo ya Spika yamekuja ikiwa ni siku chache baada ya wasemaji wa Kambi hizo kugoma kusoma hotuba zao mara mbili mfululilo katika Wizara za Habari pamoja na Mambo ya Ndani kupitia Wabunge, Joseph Mbilinyi pamoja na Mchungaji Petter Msigwa.
Akizungumza wakati wa muendelezo wa vikao vya Bunge jijini Dodoma, Spika Ndugai amesema kuwa, “naomba nizungumzie jambo moja ambalo lilijitokeza jana na siku za nyuma, hotuba za wenzetu wa upinzani kuna shida kidogo katika uandishi na wakati mwingine zinaleta matatizo makubwa, shida wanaandika nje na hawazisomi wao wanafika na kusaini tu”.
April 18, 2019 Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson aliagiza hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, iliyokuwa ikisomwa na Mbuge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kutohifadhiwa kwenye kumbukumbu za Bunge baada ya Mbunge huyo kugoma kuisoma.