Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mhimili huo wa Dola umeshamlipa madai yake yote mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu huku akimwagiza kuwa kama ana jambo lolote kuwasiliana na mamlaka husika na si kutumia mitandao ya kijamii.
“Pale bungeni hatumuonei mtu hata kidogo...wameshamlipa,” alipoulizwa amelipwa madai gani alisema, “usitake tena… yaani hana madai. Kama ana madai mengine atasema.”
Mbunge huyo amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi katika makazi yake Area D jijini Dodoma. Mpaka sasa yupo Ubelgiji akiendelea na matibabu.
Katika maelezo yake, Ndugai alisema Lissu anatumia njia zisizo nzuri kueleza masuala yake, likiwamo hilo la madai yake.
“Hii si njia nzuri ya mawasiliano. Ninachosisitiza mtu ni mtumishi katika taasisi unatakiwa kuwajibika kwa watu fulani fulani lakini huwatambui huwasiliani nao,” alisema Ndugai.
Alimshauri Lissu kutafuta ufumbuzi wa masuala yake ya bungeni kupitia viongozi mbalimbali wa upinzani.
“Haki ya mtu ni haki ya mtu, siwezi kusimama katikati ya haki ya mtu… sifuatiliagi mshahara wa mtu mmojammoja mwisho wake nitahamia uhasibu,” alisema Ndugai huku akicheka.
Credit: Mwananchi
Social Plugin