Spika wa Bunge Job Ndugai,amesema Mbunge wa Kigoma Mjini,Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) anawadanganya wananchi.
Ndugai alisema uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), unaofanywa na Zitto unalenga kuwaaminisha wananchi kwamba kila kilichomo kwenye ripoti hiyo ni cha kweli.
Alisema kwa upande wake humuungi mkono kwa kuwa ukweli wa ripoti hiyo hudhihirishwa na kamati mbili za Bunge ambazo ni kamati ya PAC na LAAC.
Spika Ndugai aliyasema hayo bungeni leo mchana muda mfupi kabla hajaahirisha Bunge hadi jioni.
Pamoja na hayo Spika alisema Zitto anatumia muda wake mwingi kuichambua ripoti hiyo kwa kuwa anataka awe Mwenyekiti wa Kamati ya PAC kinyemela.
“Kama nilivyosema wakati fulani zile ni hoja, lakini watu wanawaaminisha Watanzania kuwa kila kichoandikwa na CAG mle ni ukweli asilimia mia moja. Yapo mambo mle si kweli hata kidogo tena mengi tu.
“Mengine utakuta kiambatanisho tu hakipo na mifano ipo mingi, yaani kitabu huchambuliwa na wakati mwingine zinabaki hoja chache ndio tunawapa Serikali au polisi kama zinahusu huko. Anachokitaka Zitto ni kuendelea kuwa mwenyekiti wa PAC kinyemelela.” Amesema