Takribani watu 156 wanaripotiwa kufariki dunia na mamia kujeruhiwa kufuatia milipuko iliyotokea katika makanisa na hoteli nchini Sri Lanka.
Milipuko sita imeripotiwa kutokea katika maeneo mbalimbali nchini humo wakati raia wa nchi hiyo wakisherehekea sikukuu ya Pasaka.
Katika milipuko hiyo sita iliyotokea, milipuko mitatu imetokea katika makanisa, huku mingine mitatu ikitokea katika hoteli tatu tofauti.
Makanisa ambamo milipuko imetokea ni Kochchikade, Negombo na Batticaloa huku hoteli zilizokumbwa na milipuko zikiwa ni, The Shangri La, Cinnamon Grand na Kingsbury.
Picha mbalimbali katika mitandao ya kijamii zinaonesha hali ilivyo katika baadhi ya maeneo ambamo milipuko hiyo imetokea. Majengo yanaonekana yameharibika, pamoja na damu za watu kutapaa chini, huku vyombo vya huduma ya kwanza na Polisi wakitoa misaada.
Rais Maithripala Sirisena amewataka wananchi kuwa watulivu wakati wa kipindi hiki kigumu, na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi ili kufanikisha uchunguzi.
Viongozi wengine nchini humo wamelaani mauaji hayo ambayo yanayoonekana kuwa yalikuwa yamepangwa, na kugharimu uhai wa watu wasio na hatia.
Kwa muda kumekuwapo na vitisho vya kundi la kigaidi la ISIS nchini humo. Lakini hadi sasa hakuna kundi lolote lililokiri kuhusika na shambulio hilo.
Social Plugin