Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kuwajali wanawake , wafungwa wajawazito kwa kuwapatia huduma zote anazopaswa kupatiwa mama mjamzito.
Hayo yamesemwa April 17 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mhe.Kangi Lugola wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum mhe.Angelina Adam Malembeka aliyehoji ,baadhi ya akina mama wajawazito huingia gerezani wakiwa wajawazito na kujifungulia gerezani je,ni huduma gani hupata ili kuhakikisha anajifungua salama.
Katika majibu yake Mhe.Lugola amesema jeshi la Magereza limekuwa likitoa huduma za afya ,chanjo na kuhakikisha wanahudhuria kliniki ya akina mama wajawazito katika vituo vya afya vya magereza.
Aidha amesema jeshi la magereza limekuwa likiwapatia wafungwa wajawazito vyakula vinavyohitajika kiafya kwa kuzingatia maelekezo na ushauri wa madaktari wa Magereza.
Katika swali lake la nyongeza Mhe.Malembeka amehoji ,Serikali inawasaidiaje watoto wanaozaliwa magerezani kisaiklojia na kielimu na kwanini pasiruhusiwe vifungo vya nje kwa akina mama wajawazito na wenye watoto ili waweze kulea watoto wao vizuri.
Akijibu Swali hilo,mhe.Lugola amesema kuna utaratibu watoto wanaozaliwa Magerezani wamekuwa wakisoma shule za awali zilizoko magerezani na wanawake wafungwa wenye vifungo chini ya miaka mitatu kuna sheria ya “Probation for Offender “pamoja na sheria ya “Community Services “ ambapo pia huwa na utaratibu wa kuwaondoa wafungwa wajawazito na wenye watoto ili wawe na vifungo mbadala.
Hata hivyo watoto wanaoishi Magerezani wanapokuwa wakubwa na kufikia umri wa kuishi bila mama zao ,ndugu zao wamekuwa wakishirikishwa ili waweze kutoa malezi kwa watoto ambao mama zao wako magerezani.
Katika hatua nyingine Waziri Lugola amesema sheria,taratibu na mila za kitanzania ,Serikali haiwezi kuruhusu wafungwa walio katika ndoa kufanya mapenzi magerezani.
Social Plugin