Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ amemshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akienda Mbeya kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani asisahau kuongeza mishahara kwa watumishi wa umma kwa sababu miaka yake minne hajawahi kuongeza hata kidogo.
Sugu ametoa kauli hiyo wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Amesema kwa nidhamu kubwa anamuomba Rais atakapokuwa Mbeya atangaze ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi kwa sababu, tangu aingie madarakani na huu ni mwaka wa nne mishahara haijaongezeka.
“Wafanyakazi wana hali mbaya sana maeneo yote ya nchi hii. Pia, aangalie suala la wastaafu wapo wengi wengine ni mwaka wa pili sasa hawajalipwa mafao yao,” amesema Sugu
“Katika idara mbalimbali ikiwamo za ulinzi na usalama kama magereza, polisi ni miaka miwili sasa wastaafu wapo katika kota hawana nauli za kubebea mizigo kurudi kwao.”
Amewaomba Mawaziri kama suala la nyongeza ya mishahara halipo mezani warudi na kuangalia upya ili Rais atakapokwenda Mbeya atangaze ongezeko kwa watumishi wa umma, ili kuwezesha kupata nafuu ya maisha.
Social Plugin