Leo Jumanne tarehe 2 Aprili 2019 Bunge la Tanzania linatarajia kuanza Mkutano wa Kumi na Tano utakaomalizika tarehe 28 Juni 2019 Mjini Dodoma.
Mkutano huu utakuwa ni mahsusi kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa Bajeti za Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2018/19 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.
Katika Mkutano huo, wastani wa maswali 515 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na kujibiwa na Serikali Bungeni.
Aidha, wastani wa Maswali 88 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa kwa siku za Alhamisi.
Pia, Bunge litajadili Hotuba ya Hali ya Uchumi wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 itakayowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango.
Katika hatua nyingine Bunge pia linatarajia kujadili na kupitisha Miswada Miwili (2) ya Sheria ambayo itasomwa kwa hatua zake zote ambayo ni Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi wa mwaka 2019 (The Appropriation Bill, 2019), na Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 (The Finance Bill, 2019.
Social Plugin