Tuzo za Mo Simba zilizoasisiwa na Mohammed Dewji mwaka 2018 zinatarajiwa kutolewa kwa awamu ya pili baada ya kumalizika kwa msimu wa 2018/2019.
Tuzo za mwaka huu zitahusisha wachezaji na mashabiki wa klabu ya Simba ambao juhudi zao zimewezesha klabu kufikia mafanikio ambayo imeyapata kwa msimu wa 2018/2019.
Kwa mwaka huu kutakuwa na vipengele 11, ambavyo ni Mchezaji Bora wa Mwaka, Goli Bora la Mwaka, Golikipa Bora wa Mwaka, Beki Bora wa Mwaka, Kiungo Bora wa Mwaka na Mshambuliaji Bora wa Mwaka.
Tuzo zingine ni Mchezaji Bora Mwanamke wa Mwaka, Mchezaji Bora Mdogo wa Mwaka, Shabiki Bora wa Mwaka, Tuzo ya Heshima na Mhamasishaji Bora wa Mwaka katika Mitandao ya Kijamii.
Washindi wa tuzo hizo watatokana na kura ambazo zitapigwa na mashabiki kupitia mitandao ya kijamii, tovuti rasmi ya tuzo ambayo tutaitangaza hivi karibuni na kamati maalumu ambayo itahusisha wadau mbalimbali wa mpira wa miguu nchini.
Akizungumza kuhusu tuzo za mwaka huu, Dewji amesema tuzo hizo zitatolewa kama sehemu ya kutambua mchango wa baadhi ya watu ambao juhudi zao kubwa zimesaidia Simba kufika hapa ilipo sasa.
Amesema tuzo za mwaka huu zitakuwa na hadhi kubwa tofauti na mwaka uliopita kwani yamefanyika maandalizi makubwa ambayo yatawezesha hafla ya utoaji wa tuzo kwa mwaka huu kuwa ya kisasa zaidi na yenye kuvutia kwa watakaohudhuria na ambao wataangalia kupitia runinga.
“Tumepata mafanikio makubwa kwa msimu huu ikiwepo kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hili ni jambo kubwa kwetu na Taifa kwa ujumla na kama tulivyofanya mwaka jana na mwaka huu tena tunafanya kuwapa tuzo wote waliofanikisha Simba kufanikiwa,
“Najua kila shabiki wa Simba ana mchango wake kufanikisha sisi kufika hapa kwa maana hata kuja tu uwanjani kushangilia timu hilo ni jambo kubwa sana, lakini kwa kawaida tuzo inatolewa kwa watu wachache kati ya wengi hivyo tutachagua wachache kati yetu na kuwapa tuzo, na sisi mashabiki wenyewe ndio tutachagua,” amesema Dewji.
Tarehe ya kufanyika kwa tuzo na sehemu ambayo hafla itafanyika tutatoa taarifa hivi karibuni baada ya kutangaza vipengele na mchakato wa kupiga kura kuanza.
Imetolewa na;
Kamati ya Maandalizi ya Tuzo za Mo Simba 2019
30/04/2019
Social Plugin