Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAHADHARI YA KIMBUNGA KIKUBWA NCHINI TANZANIA

Taarifa hii inatoa mrejeo wa mwenendo wa mgandamizo mdogo wa hewa uliopewa jina la “Kenneth” katika bahari ya Hindi na athari zake kwa maeneo mbalimbali hapa nchini.


Katika kipindi cha saa 24 zilizopita, mgandamizo mdogo wa hewa (Kenneth) umeendelea kuimarika kwa kasi hadi kufikia kiwango cha kimbunga kamili. 

Kimbunga Kenneth kwa sasa kipo umbali wa takribani kilometa 700 mashariki mwa Mtwara. Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga Kenneth kilichopo eneo la kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Madagascar kinaambatana na mvua kubwa na upepo mkali katika eneo hilo.

 Aidha, vipindi vya upepo mkali unaofikia na kuzidi kasi ya kilometa 80 kwa saa vinatarajiwa kujitokeza katika ukanda wa pwani ya kusini (Lindi na Mtwara). 

Kimbunga hicho kinaendelea kutawala mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini, hivyo kusababisha ongezeko la mvua zinazoambatana na ngurumo za radi pamoja na upepo mkali kadri kinavyokaribia maeneo ya ukanda wa pwani.

Kimbunga hiki kitakapoingia nchi kavu kikiwa na nguvu inayotarajiwa kitakuwa na madhara makubwa kwa maisha ya watu na mali zao. 

Madhara yanayotarajiwa ni pamoja na mtawanyiko mkubwa wa mafuriko, uharibifu wa mali na makazi, kuezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali, uharibifu wa mazao mashambani, miundombinu kutokana na mafuriko na upepo mkali, kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari katika kipindi kifupi (storm surge), kuathirika kwa shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu inaweza kuathirika hasa katika mkoa wa Mtwara na maeneo jirani (umbali wa kilometa 500).

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kujengeka kwa kimbunga hicho kusini magharibi mwa bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo mingine ya hali ya hewa kwa ujumla na itaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zilizotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com