Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Njombe inaendelea na uchunguzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha Njombe mjini ambacho kimeshindwa kukamilika kwa wakati na kuchukua zaidi ya miaka 6 mpaka sasa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Njombe , Bw Charles Mulebya wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake.
"TAKUKURU mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu (2019) tulianza kufanya uchunguzi juu ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi inayoendelea kujengwa katika halmashauri ya mji wa Njombe, kufuatia taarifa ya ukaguzi uliofanywa na ofisi ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali na kuibua ubadhilifu katika ujenzi huo.” Alisema Bw Mulebya.
Aidha, Bw Mulebya alisema kuwa kutokana na uchunguzi wanaoufanya mpaka Sasa wamefikia katika hatua nzuri na karibuni utakamilika.
“Ujenzi huu utagharimu shilingi Bil 9.7 hadi kukamilika kwake na uchunguzi upo kwenye hatua nzuri za kukamilika, uchunguzi unafanyika kwa umakini mkubwa ili yeyote aliyehusika akutane na mkono wa sheria kwa kusababisha ucheleweshwaji wa kituo hicho pamoja na ubadhilifu wa fedha ulioibuliwa hivi karibuni.” ameongeza Bw Mulebya.
Mbali na hivyo, Kaimu huyo amebainisha kuwa uchunguzi wa majalada ya mwanzo umebaini makosa chini ya manunuzi ya umma na kanuni zake za mwaka 2013 na mara baada ya kukamilika majalada yatapelekwa makao makuu kwa hatua zaidi.
Katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, iliyofanyika kwa siku tatu mkoani Njombe, Rais alimuagiza mkurugenzi na mkandarasi wa kituo hicho cha mabasi mjini Njombe kuhakikisha mpaka mei 5 kimekamilika na kuanza kutumiwa.
Social Plugin