Na. OWM, MOROGORO.
Mtandao wa Afya moja kwa nchi za Afrika mashariki, Kati na Magharibi (OHCEA) umeendesha mafunzo ya Dhana ya Afya moja kwa wanafunzi wa ngazi ya Stashahada na Astashahada kutoka vyuo vya kwenye sekta za Afya ya Binadamu, Mifungo, Wanyamapori na Mazingira. Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Duniani kufundisha Dhana hiyo katika ngazi hizo za taaluma, kwa kuwa nchi nyingine duniani hufundisha tu kwa ngazi ya Shahada na Shahada ya Uzamivu masuala ya Afya moja.
Dhana ya Afya moja ambayo ni ushirikishwaji wa pamoja sekta ya Afya ya Binadamu, Wanyamapori, Mfugo, Kilimo na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu ama kinyume chake. Wataalamu hao wamepata mafunzo hayo kwakuwa wapo karibu sana na jamii na pindi utokeapo mlipuko wa ugonjwa ndio huwa kikosi kazi cha kwanza na mstari wa mbele kuwa eneo la tukio katika kufuatilia na kukabili milipuko, kabla ya wataalamu wengine kushiriki kikamilifu.
Akiongea wakati wa kufunga Warsha ya kufanya tathmini ya namna wakufunzi wanavyotumia mitaala ya Afya Moja katika kuwafundisha wanafunzi wao wa ngazi ya Stashahada na Astashahada, tarehe 13 Aprili, Mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe alifafanua kuwa mafunzo hayo yanajenga kikosi kazi imara chenye kuchagiza shughuli za Afya moja hapa nchini.
“Katika kuimarisha Afya ya Binadamu pamoja na Afya ya mifugo na wanyamapori, kwa kutumia Dhana ya Afya moja, ninafarijika kwa jitihada hizi za kuwajengea uwezo Wataalamu wa sekta za Afya katika ngazi ya Stashahada na Astashahada pamoja na wakufunzi wao, kwa kuwa tunaandaa rasilimali watu ya kuweza kuwa na uwezo wa kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa kwa Dhana ya Afya moja. Alisema Matamwe.
Wakiongea kwa nyakati tofauti waratibu wa mafunzo hayo Profesa; Japheti Killewo na Profesa. Robinson Mdegela walifafanua kuwa tayari mitaala ya Afya moja kwa ngazi ya stashahada na astashahada imekamilika, lakini wakati taratibu za kuingiza masuala ya Afya moja zitakamilika hivi karibuni katika mitaala ya ngazi ya stashahada na Astashahada wameamua kufanya mafunzo hayo ili wakufunzi kujifunza kwa vitendo juu ya kufundisha masuala ya Afya moja lakini pia na kuwaandaa wanafunzi watakao fundishwa kwa kutumia mitaala hiyo.
Aidha waratibu hao walibainisha kuwa wanafunzi hao wakiweza kuielewa vizuri dhana ya Afya moja watatumika vyema kuielimisha jamii juu ya masuala ya Afya Moja, na nchi yetu itaweza kuzuia maambukizi ya magonjwa ya mlipuko hususani yale yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu na pia kupunguza usugu wa madawa kwa sababu wataweza kuongeza ushirikiano, mawasiliano na uratibu baina ya sekta husika.
Mafunzo hayo yaliyowajumuisha zaidi ya wanafunzi 210, wa ngazi ya astashahada na ngazi ya cheti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili, SUA, Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Morogoro, Chuo cha Afya cha Kilosa, Chuo cha Wanyamapori Pasiansi na Chuo cha Wanyamapori Mweka,
Aidha, wakufunzi zaidi ya 30 wameshiriki kutoka Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine, Vyuo vya Afya Lindi, Mafinga, Kilosa, Mtwara, Singida, Kagemu, Mirembe, Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Morogoro, Temeke, Tengeru, Buhuri, pamoja na Vyuo vya Taaluma ya Wanyamapori , Pasiansi na Mweka.
Mafunzo hayo yameratibiwa na Chuo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine kwa kushirikiana na USAID, kupitia vyuo vikikuu vya MINNESOTA na Tufs vya nchini Marekani
Social Plugin