Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imesema imeweka mipango maalum ya kuboresha tasnia ya ngozi hapa nchini ili kuiongezea thamani kwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa zinazotokana na ngozi kupitia viwanda villivyopo hapa nchini.
Akizungumza na wadau wa sekta ya ngozi jijini Dar es Salaam (09.04.2019) katika ofisi ndogo za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel, amesema wizara imekuwa ikihakikisha inasikiliza na kuelewa changamoto, ushauri na fursa wanazokutana nazo wadau wa sekta mbalimbali ili wizara iweze kutekeleza kwa kasi yale yenye tija kwa ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Ni lazima tuhakikishe tunaongeza thamani katika bidhaa zetu za ngozi, hili ni jambo kubwa ambalo tutakuwa tumeunga mkono azma ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi unaoendana na kukua kwa viwanda ili tasnia ya ngozi ipate viwanda vingi, ni vyema tuongeze thamani badala ya kuuza ngozi tuuze bidhaa zitokanazo na ngozi.” Amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel amewataka pia watanzania kubadili fikra kwa kutumia bidhaa za ngozi zinazotengenezwa hapa nchini kwa kuwa zina bei nafuu na zinadumu kwa muda mrefu ili wazalishe wawe na soko kubwa la ndani kabla ya kuuza nje ya nchi huku akiwataka pia watengenezaji wa bidhaa hizo kutengeneza zenye ubora zaidi ili ziweze kupata masoko ya uhakika.
Aidha katibu mkuu huyo amesema ni vyema yawepo maboresho ya mitaala ili kupata wataalam wa ngozi ambao watawasaidia wadau na wananchi katika nyanja mbalimbali zihusuzo tasnia ya ngozi yakiwemo masoko.
Ili tasnia ya ngozi izidi kukuza uchumi wa taifa Prof. Gabriel amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikihakikisha inasimamia ubora wa ngozi ya ng’ombe kuanzia kwenye mbegu bora ya ng’ombe inayoweza kuzalisha ngozi bora.
“Katika wizara yetu hatushughuliki tu na mnyama ambaye tayari amezaliwa anakaribia kuchinjwa sisi tunaanza na mbegu yenyewe kwanza ili kuhakikisha mnyama anayezaliwa anakuwa na ngozi bora na kuhakikisha anatunzwa au kutayarishwa ili atoe ngozi bora.”
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa ngozi nchini Bw. Joram Wakari amesema tasnia ya ngozi imekuwa na changamoto kadhaa ambazo tayari Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikizitatua hivyo kuiomba wizara kuzidi kusimamia tasnia ya ngozi ili iweze kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa taifa.
Baadhi ya wadau walioshiriki katika mkutano huo wameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa jitihada ambazo viongozi wake wamekuwa wakifanya kwa kukutana na wadau wa sekta mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha wanapata maoni na ushauri wa namna ya kuendeleza sekta hizo kwa kushirikiana na wananchi.
Mwisho.
Social Plugin