Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TUNDU LISSU KUREJEA TANZANIA MUDA WOWOTE


Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amesema muda wowote atareja nchini kutokea matibabuni nchini Ubelgiji.

Lissu  amesema kuwa tayari  madaktari wake wamemueleza ni siku gani atakuwa tayari kurejea nchini.

Hata hivyo Lissu ameeleza kuwa wanahitaji kushauriana na wadau mbali mbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwake nyumbani.


"Tarehe 2 ya mwezi huu nilikutana na madaktari wangu kwa appointment ya kwanza tangu operesheni za tarehe 20 Februari.

"Taarifa yao ni kwamba mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa 'kiraka' cha mfupa na kupigwa 'ribiti' ya chuma juu kidogo ya goti; na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri.

"Sasa kazi kubwa iliyobaki ni kukunja goti na kujifunza kutembea tena. Naomba mniamini nikisema kujifunza kutembea tena, baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa kulala kitandani, ni kazi ngumu sana!!!!

"Nafikiri sina tofauti sana na mtoto mdogo anayejifunza kupiga hatua zake za kwanza. Lakini pole pole nitafika inshaallah.

"Tarehe 14 ya mwezi ujao nitapimwa urefu wa miguu ili nitengenezewe kiatu au soli maalum kwa ajili ya mguu wa kulia.

"Kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, mguu huo ni mfupi kwa sentimita kadhaa. Bila kiatu au soli maalum nitakuwa 'langara' sana na madaktari wamesema hiyo sio sawa sawa.

"Kwa kumalizia, sasa nina tarehe ambayo madaktari wangu wamesema nitakuwa 'fiti' kurudi nyumbani.

"Msiniambie niiseme kwa wakati huu. Tunahitaji kushauriana na wadau mbali mbali kuhusu tarehe halisi na namna bora zaidi ya kurudi kwangu nyumbani.

"Tukumbuke tu kwamba waliotaka kuniua mchana kweupe katikati ya mji wa Dodoma bado wanaitwa 'watu wasiojulikana.' Itabidi tupate 'security guarantees' kutoka kwa wahusika,  kwamba nitakuwa salama nikirudi." Amesema Tundu Lissu katika waraka wake aliouweka mtandaoni


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com