Mpendwa Msomaji wetu, Jana Ijumaa April 19,2019 tulichapisha Habari inayohusu ujenzi wa Stendi ya Mabasi Njombe iliyokuwa na kichwa cha habari; "Mwanzinga: Agizo La Rais Magufuli Kukamilishwa Kituo Cha Mabasi Njombe Mjini Ndani Ya Siku 30 Haliwezi Kufanikiwa."
Habari hiyo ilinukuu mahojiano kati ya mwandishi wetu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Ndg. Edwin Mwanzinga kuhusu maendeleo ya ujenzi wa stendi mpya ya Njombe na namna walivyojipanga kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. John pombe Magufuli ambaye April 10, 2019 aliagiza ujenzi wa kituo hicho ukamilike ndani ya siku 30.
Hata hivyo, katika mahojiano hayo, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Njombe Ndg. Edwin Mwanzinga kuelezea maendeleo ya mradi huo, lakini alinukuliwa vibaya kwamba ujenzi huo unaweza usikamilike kwa asilimia 100 ndani ya muda walioagizwa na Rais Magufuli.
Tunaomba radhi kwa makosa hayo ya kiufundi yaliyojitokeza.
Uhalisia wake ni kwamba, Ndg. Edwin Mwanzinga alifafanua kuwa stendi hiyo itakamilika kwa mujibu wa tarehe ya mkataba ambayo ni 30/04/2019 na shughuli zitakazosalia za ukamilishaji zitafanyika ndani ya siku zilizoongezwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kama alivyoagiza kwenye ziara yake ya kikazi tarehe 10 Aprili akiwa Mkoani Njombe ambapo ni kufikia tarehe 10, Mei 2019.
Ujenzi wa kituo hicho cha mabasi unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 9 ulianza kujengwa tangu mwaka 2013.
Social Plugin