UJENZI WA MRADI WA MAJI MAGU WAFIKIA ASILIMIA 85


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA), Mhandisi Anthony Sanga amesema ujenzi wa mradi wa maji katika Mji wa Magu, Mkoani Mwanza umefikia asilimia 85 za ujenzi wake.


Mhandisi Sanga alisema hayo alipofanya ziara kwenye mradi huo Aprili 24 kwa lengo la kujionea na kujiridhisha hatua iliyofikiwa ya ujenzi wake ambao unasimamiwa na MWAUWASA kwa niaba ya Wizara ya Maji.

Mhandisi Sanga alisema utekelezaji wa jumla wa mradi umefikia asilimia 85 na ulazaji wa bomba kwa ajili ya kuunganisha wananchi imefikia asilimia 95.

Alibainisha kwamba mradi una uwezo wa kuzalisha lita 7,250,000 ambayo ni mahitaji ya Mji wa Magu kwa miaka 20 ijayo. “Mradi huu ni mkubwa sana hata kama wananchi wa Magu wataongezeka mara mbili zaidi bado utaweza kuwahudumia,” alisema Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga alisema kukamilika kwa miradi inayotekelezwa chini ya ufadhili wa Serikali kupitia mpango wa Uboreshaji wa Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Ziwa Victoria, miji yote mikuu ya Mkoa wa Mwanza itakua imepata huduma ya majisafi na salama kutoka Ziwa Victoria.

“Mradi ukikamilika miji yote mikuu ya Mkoa wa Mwanza itakua imepata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria kwani tumepeleka Nansio, Sengerema, Ngudu, Magu na Misungwi,” alisema.

Mhandisi Sanga aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na wa Wilaya ya Magu kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwenye shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi.

Aidha, aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano wanaoutoa hususan wa ulinzi wa miundombinu ya maji inayotumika kwenye ujenzi wa mradi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم