Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UMOJA WA MATAIFA WALAANI MATUMIZI YA SILAHA NZITO LIBYA


Ujumbe wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa Libya umelaani ongezeko la matumizi ya silaha nzito na mashambulizi holela dhidi ya makazi ya watu, shule na miundombinu na kutaka huduma za dharura kuwafikia raia waliokwama.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM, idadi ya watu wasio na makazi ndani na nje ya mji wa Tripoli hivi sasa inakaribia 20,000. Zaidi ya watu 2,400 walikimbia makazi yao katika kipindi cha masaa 24 pekee.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujaric, amewaambia waandishi wa habari jijini New York kwamba familia nyingi zinazokimbia maeneo yaliyo na machafuko zinaelekea katikati mwa Tripoli na maeneo ya karibu, lakini takribani watu 14,000 wasio na makazi wametafuta hifadhi nje ya mji huo mkuu katika maeneo ya Tajoura, Al Maya, Ain Zara na Tarhouna.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana lilianza kujadili azimio lililoandaliwa na Uingereza la kutaka kusitishwa mapigano nchini Libya, baada ya majeshi tiifu ya kamanda Khalifa Haftar kuanzisha mashambulizi mjini Tripoli.

Mapigano mapya nchini Libya yalizuka kiasi wiki mbili zilizopita wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres, baada ya kiongozi wa vikosi vya mashariki Jenerali Khalifa Haftar kuanzisha operesheni ya kuchukua udhibiti wa mji mkuu Tripoli na kukabiliana na upinzani wa vikosi vya serikali inayotambuliwa kimataifa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com