Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza amemvaa Katibu Mwenezi wa CCM, Humphery Polepole, kuwa amewadhalilisha wabunge wa viti maalumu wanaotokana na chama chake kuwa wamepata nafasi hizo baada ya kufanya ngono na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Peneza ameyasema hayo jana Jumatano Aprili 17, 2019 akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Amesema wabunge wa viti maalumu wapo kwa mujibu wa Katiba lakini kuna kitu kibaya kilianza kutokea ndani ya Bunge na kwamba, viongozi wa Bunge wanapokaa kuendesha Bunge wamekuwa wakikemea tabia hiyo aliyoita ni ya kipuuzi.
"..Mwenyetiti na viongozi wengine wa Bunge walikemea tabia hii ya "kipuuzi", lakini sasa imefika huko nje ambapo ndugu, Humphrey Polepole amesema wabunge wa viti maalum wa CHADEMA wanapatikana mpaka "wapitiwe" na Mwenyekiti wao, huu ni udhalilishaji.
“Sasa kama hata hatambui haki za kikatiba ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na mwenezi anayedhalilisha wanawake… lakini ifike mahali nafasi walizonazo na vyeo walivyonavyo viheshimiwe,” amesema.
Amesema ni aibu kwa kiongozi kusimama na kusema kuwa nafasi ya mwanamke kisiasa inatokana na ngono.
"Ni aibu kwa kiongozi wa nchi hii kusimama na kusema kwamba mafanikio ya mwanamke ya kisiasa yanatokana na shughuli za kingono, tunawajengea watoto wetu fikra mbaya ndani ya kichwa chao" Amesema Peneza
Social Plugin