Wanajeshi wanaotawala kwa sasa Sudan na makundi ya upinzani ya nchi hiyo wamefikia makubaliano ya kubuni Baraza la Pamoja kwa ajili ya kuendesha masuala ya nchi hiyo.
Akitangaza habari hiyo, Ahmad ar-Rabii' mmoja wa wakilishi wa makundi ya upinzani amesema kwamba katika kikao chao kilichofayika jana Jumamosi mjini Khartoum, wapinzani na Baraza la Kijeshi wamekubaliani umuhimu wa kubuniwa Baraza la Pamoja la wanajeshi na wapinzani kwa ajili ya kuendesha kwa muda masuala ya Sudan.
Ar-Rabii' ambaye alihudhuria kikao hicho amesema kwamba mazungumzo yangali yanaendelea kuhusu kuainishwa kwa idadi ya wanajeshi na wapinzani watakaojumuishwa katika baraza hilo la pamoja.
Kikao hicho cha pamoja kati ya wanajeshi na wapinzani kimefanyika siku moja baada ya muungano wa upinzani kwa jina la 'Makundi Yanayopigania Uhuru na Mabadiliko' kutangaza habari ya kubuniwa ujumbe wa wapinzani kwa ajili ya kufanya mazungumzo na wanajeshi.
Baraza la Kijeshi la Sudan lilibuniwa baada ya Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo kung'olewa madarakani na wanajeshi tarehe 11 Aprili.
Baraza hilo lilikuwa limetangaza awali kwamba lingetawala kwa muda wa miaka miwili kabla ya kukabidhi madaraka kwa raia.
Wananchi na makundi ya upinzani wamekuwa wakifanya maandamano na mgomo mbele ya makao makuu ya wanajeshi mjini Khartoum kwa ajili ya kushinikiza raia wakabidhiwe madaraka nchini.