Jamii ya watu wa Ilimanyang inayopatikana nchini Kenya, ni jamii ya watu wenye utofauti mkubwa na jamii zingine kutokana na watu wake kukosa vitu vya muhimu.
Watu hao ambao wanapatikana katika kijiji cha Kapua jimbo la Turkana nchini Kenya, hawana matundu ya kutoa jasho katika ngozi zao, kitu kinachowaletea shida kubwa ya joto na kuwalazimu kutembea na vyombo vya maji ili kujimwagia mwilini kila mara ili kupooza makali ya joto.
Suala hilo limekuwa changamoto zaidi kwa watoto wa shule, ambao hulazimika kutoka nje ya madarasa yao mara kwa mara ili kujimwagilia maji, kupooza joto kali la mwili.
Si hilo tu la kukosa vitundu vya kutolea jasho, bali watu hao pia hawana nywele na meno kabisa kama ambavyo binadamu wengine tunayo, hivyo hushindwa kula baadhi ya vyakula.
Mwana Ilimanyang anasimulia
Mmoja wa wakazi wa jamii hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Peter Lomonta amesimulia kuwa, "Sisi hatuna nywele, hatuna meno, hatutoki jasho, ukisimama juani mwili unakuwa wa joto sana inabidi upooze na maji, watoto wetu wanapata shida sana wakienda shule, wakipewa mahindi hawawezi kula hivyo wenzao huwasukuma sukuma na kumwaga maji yao, hivyo wakipigwa na jua mwili unapata moto sana wanakufa, sisi tunakufa, tunaisha, serkali itusaidie”.
Mtaalamu wa masuala ya afya na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Lodwar, Dkt. Stephen Akitela, amesema tatizo hilo huwa ni la kuzaliwa nalo, na mara nyingi huwapata vijana wa kiume. Ila watu hao wanapokwenda hospitali hutibiwa kwa magonjwa husika ambayo mgonjwa ameenda kuelezea, na sio kama ipo dawa ya kuweza kumpa akabadilika na kuwa kama binadamu wengine.
Chanzo: BBC