Agizo la Rais John Magufuli limesababisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, na wasaidizi wake kuhamia kwenye ofisi za mabati mjini Dodoma.
Jaffo na manaibu waziri wake wawili, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na watumishi wengine wamelazimika kuhamia kwenye ofisi za muda za mabati hayo kutekeleza agizo lililotolewa na Rais Magufuli mwishoni mwa wiki.
Jengo la ghorofa mbili la wizara hiyo lililopo kwenye mji wa serikali uliopo Mtumba jijini hapo halijakamilika, hali iliyomkera Rais Magufuli ambaye aliwataka wahamie hivyo hivyo.
Mbali na mawaziri hao, pia baadhi ya Idara muhimu za wizara hiyo zimehamia kwenye ofisi hizo za mabati, huku mafundi wakiendelea na ujenzi wa jengo ambalo walipaswa kuwamo.
Rais Magufuli mwishoni mwa wiki alizindua mji huo ambapo aliagiza wizara zote 23 kuhakikisha zinahamia eneo hilo zikiwamo tatu ambazo hazijakamilisha majengo yake.
Jafo amesema walihamia tangu Jumatatu yeye pamoja na manaibu wake, Katibu Mkuu na baadhi ya idara muhimu.
Amesema wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika ofisi yao hiyo mpya, huku mafundi wakiendelea na ujenzi ambao unatarajiwa kukamilika Mei 30, mwaka huu.
“Nilipokuwa nakuja hapa, kuna watu walikuwa wananishangaa wakiwamo mafundi wetu ambao waliniambia ofisini kuna joto, mimi najiona nipo sawa,” alisema.
Jafo alisema yeye anashinda vijijini kukagua miradi ya maendeleo hivyo katika mazingira hayo ya sasa ya mabati anaona ni jambo la kawaida tu.
Hata hivyo, Jaffo alisema jengo lake ni kubwa la ghorofa mbili na ni miongoni mwa majengo ya kisasa ambayo baada ya kukamilika litakuwa linavutia.
Jafo alisema litakuwa na uwezo wa kuchukua watumishi 88, kutakuwa na kumbi mbili za mikutano ambao mmoja utachukua watu 25 na ukumbi mkubwa utakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 60.
Social Plugin